Habari Mseto

KeNHA yafungua barabara iliyofurika

January 14th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MAMLAKA ya Kitaifa Kusimamia Barabara Kuu Kenya (KeNHA) imefungua upya barabara ya Kaplong-Kisii, baada ya kufungwa kwa muda kutokana na mafuriko.

Mamlaka hiyo ilifunga barabara hiyo Jumamosi, baada ya mvua kali iliyokuwa ikinyesha katika eneo hilo kuiharibu na kuifanya kutopitika.

Mvua hiyo iliharibu kabisa eneo la Mugeni, lililo karibu na Sotik na Chebilat, hali iliyoilazimu mamlaka kuifunga.

Hata hivyo, kwenye taarifa Jumapili, Desemba 14, 2024 KeNHA ilisema uamuzi wa kufungua upya barabara hiyo ulifikiwa baada ya kiwango cha maji kupungua katika daraja la Mto Kipsonoi, eneo la Mugeni.

“KeNHA imefungua barabara ya Kaplong-Kisii. Hili ni baada ya maji katika Daraja la Mto Kipsonoi kupungua, eneo la Mugeni. Tumetathmini hali ya daraja hilo na kubaini haikuharibiwa kwa vyovyote vile na mafuriko yaliyotokea,” ikaeleza mamlaka hiyo kupitia taarifa.

Ikaongeza: “Madereva wameraiwa kuwa waangalifu kwa kufuata taarifa tunazotoa kuhusu hali ya barabara zetu. Waendeshe magari kwa uangalifu.”

Mvua kubwa ilisababisha mafuriko katika Daraja la Mto Kipsonoi, hali iliyoilazimu mamlaka hiyo kuchukua hatua za haraka.

“Maji yamefunika kabisa daraja, hali ambayo imefanya eneo hilo kutokuwa salama,” ikatahadharisha mamlaka hiyo.

Kutokana na tukio hilo, wafanyakazi wa mamlaka hiyo walifika hapo mara moja na kuanza kufuatilia mkondo wa maji.

Pia walikuwa wakitoa mwongozo na tahadhari kwa madereva.

Wiki iliyopita, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya ilisema kuwa kati ya Januari 14 na 20, kutakuwa na mvua kubwa katika maeneo ya Magharibi, Nyanza (ukanda wa Ziwa Victoria), Kati, Nairobi, Kusini Mashariki na Pwani.