Habari za Kitaifa

Kenya kutumia Sh14.2 bilioni kuchapisha noti mpya za pesa

Na EDWIN MUTAI August 22nd, 2024 2 min read

KENYA imetia saini makubaliano na kampuni ya Giesecke+Devrient Currency Technologies (G+D) itakayochapisha noti mpya kuchukua nafasi ya zile kuukuu au zilizoharibika, Benki Kuu ya Kenya (CBK) imefichua.

Gavana wa benki hiyo Kamau Thugge Jumatano, Agosti 21, 2024 aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kwamba kampuni hiyo italipwa Sh14.2 bilioni kutekeleza kibarua hicho ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Kampuni hiyo ya G+D itachukua nafasi ya ile ya De La Rue kutoka Uingereza ambayo, kwa miaka mingi, imekuwa ikipewa zabuni ya kuchapisha noti zinazotumika kama pesa za Kenya.

Dkt Thugge aliambia kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani, kwamba kampuni hiyo ya Ujerumani iliteuliwa kupitia mchakato wa siri kutokana na hofu ya kupungua kwa noti nchini hali ambayo ingesababisha madhara ya kiuchumi na kiusalama nchini.

“Ilibidi mchakato wa utoaji zabuni kwa njia hiyo uzingatiwe ili kuzuia uwezekano wa Kenya kukumbwa na uhaba wa noti. Sheria ya Uagizaji Bidhaa na Huduma za Umma ilizingatiwa na zabuni hiyo ikaidhinishwa na Baraza la Kitaifa la Usalama, Baraza la Mawaziri na Afisi ya Mwanasheria Mkuu,” Dkt Thugge akaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo alipofika mbele yao katika ukumbi mmoja wa jumba la Bunge Towers, Nairobi.

“Uchapishaji noti hizo ungegharimu Dola 109,422, 740 za Amerika au Sh14.2 bilioni, kwa kuzingatia thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya Dola ya Amerika wakati wa kutiwa saini kwa zabuni hiyo,” Gavana huyo wa CBK akaongeza.

Noti hizo zitakuwa na sahihi ya Dkt Thugge mwenyewe na Katibu wa Wizara ya Fedha Chris Kiptoo.

Mwaka wa kuchapishwa kwazo utakuwa 2024 na kila noti, ya thamani mahsusi, itakuwa na uzi wa kipekee wa usalama wenye uwezo wa kubadilika rangi.

CBK ilisema kuwa mapambo mengine kwenye noti hizo yatafanana na yale yaliyochapishwa 2019.

Kampuni ya kuchapisha pesa ya De La Rue- yenye asilimia 40 ya hisa za serikali ya Kenya—ilisitisha shughuli zake nchini mnamo Machi 2013 kwa kukosa zabuni mpya.

Kampuni hiyo ilitumia Sh2.48 bilioni za kulipa wafanyakazi wake 300 iliyowaachisha kazi, kulipa mawakili na kunadi mali yake.

Dkt Thugge alisema CBK ilianza kusaka mchapishaji mwingine wa noti baada ya De La Rue kuondoka nchini.

“De La Rue ilichapisha noti za Kenya, za mwaka wa uchapishaji wa 2019, hadi Januari 2023 kabla ya kuondoka Machi mwaka huo,” akaeleza.

“Katikati mwa 2023, CBK iligundua kuwa nchi ilikuwa ikikumbwa na hatari ya kuishiwa na noti. Uhaba wa noti za thamani ya Sh1, 000 ulikuwa unanukia,” Dkt Thugge akaeleza.

CBK ilifichua kuwa chini ya kandarasi hiyo ya miaka mitano, Kenya itapokea jumla ya noti 2.04 bilioni za thamani mbalimbali kuchukua mahala pa zile kuukuu au zilizoharibika.

Dkt Thugge aliambia kamati hiyo kwamba wakati huu kuna jumla ya noti bilioni 330 zinazotumika nchini.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga