Habari za Kitaifa

Kenya yathibitisha kisa cha kwanza cha homa ya tumbili

Na TAIFA RIPOTA July 31st, 2024 1 min read

KENYA imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya homa ya tumbili inayofahamika kama Monkey Pox (Mpox) katika mpaka wa Taveta na Tanzania.

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya.

Maambukizi, ambayo husababishwa na virusi vya mpox, huenea watu wanapotangamana kwa karibu, na husababisha dalili za mafua na upele.

Wizara ya Afya haikutoa habari zaidi kuhusu mtu huyo. Hata hivyo, iliwashauri Wakenya kuwa waangalifu na kunawa mikono mara kwa mara ili kupunguza hatari ya kuambukizwa.

“Nawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji. Ikiwa una dalili yoyote inayohusiana na virusi hivyo, pata ushauri kutoka kwa kituo cha afya kilicho karibu nawe na epuka kutangamana kwa karibu na watu wengine,” Wizara ilisema katika taarifa.

“Maambukizi yanaweza kutokea iwapo umetangamana au kugusa mwili wa mtu aliye na virusi hivyo kama vile kupitia mdomoni au kwenye sehemu za siri. Ugonjwa huo pia unaweza kuambukizwa kupitia matone ya kupumua.”

Virusi hivyo vimeenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na maeneo ya misitu katika Afrika Mashariki, Kati na Magharibi.