Habari Mseto

Kijana aliyeshtakiwa kumzaba polisi kujua leo ikiwa ataachiliwa kwa dhamana

June 7th, 2024 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kiufundi (TUK) Ian Ngige Njoroge anayekabiliwa na kesi ya kumnyang’anya polisi kimabavu, atarudishwa kortini leo Ijumaa kujua ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Hakimu Mwandamizi, Bw Ben Mark Ekhubi, aliamuru Ngige arudishwe gereza la Viwandani baada ya kupokea mawasilisho ya mawakili na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP), Bw Renson Igonga.

DPP alipinga Ngige kuachiliwa kwa dhamana, akisema atatoroka kukwepa adhabu kali itakayotolewa endapo atapatikana na makosa ya kumnyang’anya kimabavu Koplo Jacob Ogendo simu aina ya Samsung Galaxy yenye thamani ya Sh50,000 mnamo Juni 2,2024.

DPP kupitia viongozi wa mashtaka Victor Owiti, James Gachoka na Virginia Kariuki walipinga vikali kuachiliwa kwa dhamana kwa Ngige wakisema “kitendo hicho cha kumchapa afisa wa kudumisha usalama kimedhalilisha idara ya polisi.”

Bw Owiti aliomba mshtakiwa anyimwe dhamana iwe funzo kuu kwa wakenya wengine walio na mawazo sawa na hayo ya Ngige.
“Kitendo cha mshtakiwa kimedhihirisha jinsi anavyodharau maafisa wa kudumisha usalama.”

Kiongozi huyo wa mashtaka alimweleza Bw Ekhubi kwamba “Koplo Jacob Ogendo hakustahili kichapo alichopata hata kama aliitisha hongo ya Sh10,000 kama inavyodaiwa.”

Tamko hilo lilizua mjadala mkali baina ya mawakili Duncan Okatchi, Suyianka Lempaa na Ken Echesa waliosema “mlalamishi na maafisa wa polisi wako na mazoea ya kudai hongo kwa wenye magari, pikipiki na hata waendesha baiskeli.”

Lakini Owiti alimtetea Koplo Ogendo akisema ukweli utadhihirika siku ile atakapofika mahakamani kueleza kilichojiri.

Ngige amekana mnamo Juni 2, 2024 katika eneo la Kasarani alimnyang’anya kimabavu simu na kumpiga na kumjeruhi.

Koplo Ogendo aliokolewa na wananchi waliomtimua mbio mshtakiwa wakitisha kumfunza kilichotoa kanga manyoya.

Mahakama ilielezwa kwamba usalama wa mshtakiwa haupo tena kwa vile amezua uhasama kati yake na umma.

“Endapo mshtakiwa ataachiliwa kwa dhamana huenda akashambuliwa na umma na kujeruhiwa. Polisi wataenda kuokota maiti iwapo Ngige atashambuliwa na wananchi,” alisema wakili Danstan Omari anayemwakilisha Koplo Ogendo.

Madai hayo yalikera mawakili Lempaa na Okatchi “waliosema ni aibu na fedheha kuu kwamba polisi wanaolipwa na kodi ya mshtakiwa na wananchi wengine hawawezi kumpa ulinzi.”

Mshtakiwa alidai alichapwa na polisi na maafisa wa idara ya magereza na kumjeruhi.