Habari Mseto

Kisa cha mwanajeshi kupoteza Sh1.5 milioni akiponda raha na kidosho aliyemtilia ‘mchele’ Jijini Eldoret   

Na TITUS OMINDE August 28th, 2024 1 min read

MWANAJESHI amedai kupoteza Sh1.5 milioni baada ya kujivinjari na mwanadada mmoja wikendi.

Afisa huyo ambaye jina lake tumelibana, aliripotiwa kusafiri kutoka Nairobi ili kujiliwaza katika jiji jipya la Eldoret.

Hatimaye, alikutana na mrembo mmoja ambapo walianza kujiburudisha katika kilabu kama wapenzi.

Haukupita muda mrefu wawili hao walifahamiana kiasi kwamba mwanamke husika alianza kutumia simu ya mwanajeshi huyo.

Marafiki hao wawili waliondoka katika kilabu hiyo mwendo wa saa tisa usiku, kabla ya mwanamume huyo kurejea hapo akitaka kuonyeshwa picha za CCTV baada ya kujipata peke yake kwenye chumba walichokodi kujivinjari pamoja.

Inasemekana aligundua kuwa zaidi ya Sh300, 000 zilikuwa zimetolewa kutoka kwa simu yake ya rununu.

Baadaye, afisa huyo aligundua hakupoteza pesa zake tu kutoka kwa simu ya rununu, lakini pia alipoteza pesa zake zilizotolewa benki kupitia kwa simu yake hiyo.

Mwathiriwa pia anadaiwa kupoteza pesa zingine kutoka kwa akaunti yake ya benki ya ABSA kupitia ATM.

Kulingana na ripoti iliyotolewa katika kituo cha polisi cha Eldoret, mwanamume huyo alidai kupoteza zaidi ya Sh1.5 lioni.

Kinachoshangaza, afisa huyo alisitasita kuruhusu polisi kuanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo, akidai kuwa litakuwa na matokeo mabaya kwa familia yake.

“Nimepoteza zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mwanamke ambaye nilikuwa nikiburudika naye. Pamoja na hasara hiyo sitaki kutoa ripoti rasmi kwa sababu tukio hili linaweza kuumiza familia yangu. Natumai nitashughulikia suala hili kibinafsi kama afisa. Hivi karibuni nitamkamata mshukiwa,” afisa huyo aliambia afisa mmoja ambaye alikuwa tayari kuanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mwaka jana, 2023, kamanda wa polisi Kaunti ya Uasin Gishu alitoa amri ya kuanzishwa uchunguzi katika klabu moja mjini Eldoret (sasa Jiji la Eldoret), ambapo kulikuwa kumeripotiwa visa vya watu kuibiwa baada ya kutiliwa ‘mchele’.

Kufikia sasa, kuna zaidi ya kesi tano ambazo zinaendelea katika mahakama ya Eldoret kuhusiana na visa vya watu kuwekewa ‘mchele’.