Habari

Kitendawili cha kutoweka kwa ndege Aberdares

June 6th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

NI zaidi ya saa 21 tangu ndege inayomilikiwa na kampuni ya FLYSax ipotee Jumanne jioni ilipokuwa ikielekea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.

Shughuli za kutafuta ndege hiyo, abiria wote wanane  na marubani wake  wawili wa kike waliokuwa ndani kufikia sasa zimelemazwa na hali mbaya ya anga.

Hadi sasa imebainika kwamba ndege hiyo aina ya C2o8, yenye nambari ya usajili 5Y-CAC ilianza safari ya angani kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Kitale katika Kaunti ya Trans-Nzoia Jumanne na safari hiyo ilitarajiwa kuchukua muda wa saa moja na robo kwa kutua JKIA saa 5.30 jioni.

Hata hivo kinaya kikubwa ni kwamba kulingana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KCAA) na kampuni ya FLYSax, ndege hiyo ilionekana maeneo ya uwanja wa JKIA saa hiyo hiyo iliyotarajiwa kutua.

Hata hivyo Shirika la huduma kwa wanyamapori (KWS) ambalo ni mojawapo ya wanaoshiriki shughuli za kusaka ndege na uokoaji lilisema kwamba kulikuwa na ishara tosha kwamba ndege hiyo ilianguka  katika mlima wa Aberdares Kaunti ya Nyandarua, eneo la Njabini.

Wengine wanaoshiriki shughuli za utafutaji ni KCAA na shirika linalochunguza ajali za angani nchini.

Hadi sasa hali ya abiria na marubani hao haijulikani huku juhudi zinazotiwa na waokoaji wanaotajiwa kutoa taarifa rasmi  watakapofika eneo la ajali  zikikabiliwa na changamoto ya  hali mbaya ya anga katika mlima huo.

Ingawa hivyo, kizungumkuti kuhusiana na ajali hiyo ni ujumbe wa kuhitilafiana kutoka kampuni ya FLYSax na KCAA haswa kuhusu saa ndege ilitoka Kitale na ilipoonekana maeneo karibu na uwanja wa JKIA.

Kitendawili kingine ni  jinsi ndege hiyo ilivyofikia maeneo ya mlima Aberdare ambayo ni hatari kutokana na hali mbaya ya anga inayoshuhudiwa eneo hilo.

Habari zilizofikia tovuti ya Taifa Leo zilidai kwamba ndege hiyo ilikuwa itue uwanja wa Wilson awali lakini hilo likabadilika na ikaelekezwa  uwanjanI JKIA kutokana na sababu ambazo hazijulikani.

Kulingana na rubani ambaye hakutaka jina lake linukuliwe, ndege hiyo ilifaa kufika JKIA kupitia eneo la Utawala ndiposa ikalazimika kubadili mkondo wake hadi ikapitia njia ya Kinangop.