Michezo

Klopp na Ancelotti nguvu sawa

June 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool alikuwa mwingi wa sifa kwa Alisson Becker baada ya kipa huyo mzawa wa Brazil kufanya kazi ya ziada katika sare tasa waliyoisajili dhidi ya Everton kwenye gozi la Merseyside mnamo Juni 21, 2020.

Alisson alipangua kombora alilovurumishiwa na Dominic Calvert-Lewin ndani ya kijisanduku kabla ya kudhibiti fataki nyinginezo alizoelekezewa na Tom Davies na Richarlson de Andrade mwishoni mwa kipindi cha pili ugani Goodison Park.

“Alisson alituokoa. Matokeo yake katika gozi la leo yalikuwa katika kiwango tofauti. Hivyo ndivyo makipa wa haiba kubwa kufu yake walivyo. Watasalia langoni kwa takriban dakika 90 bila ya kuonekana kufanya chochote, lakini kazi yao itajidhihirisha yenyewe nyakati muhimu kama hizi,” akasema Klopp.

Liverpool kwa sasa wanahitaji alama tano kutokana na mechi nane zilizosalia msimu huu ili kutia kibindoni ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Hata hivyo, huenda masogora hao wa Klopp wakatawazwa mabingwa wa muhula huu watakaposhuka dimbani kuvaana na Crystal Palace uwanjani Anfield mnamo Juni 24 iwapo Manchester City watashindwa kuchabanga Burnley ugani Etihad.

Liverpool walikosa huduma za fowadi Mohamed Salah na beki Andy Robertson katika mchuano huo uliowashuhudia wakikosa kabisa kubisha lango la kipa Jordan Pickford licha ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kuonekana kuwazidi Everton maarifa katika takriban kila idara.

Hofu ya Liverpool kwa sasa inasalia kuwa majeraha yatakayowaweka nje James Milner na Joel Matip katika mechi mbili zijazo dhidi ya Palace na Man-City. Hata hivyo, afueni kubwa kwa Klopp ni ufufuo wa makali ya Naby Keita na Joe Gomes watakaojaza nafasi za wawili hao.

Everton ambao kwa sasa wananolewa na kocha Carlo Ancelotti walisalia kuibana sana safu yao ya kati kila mara walipovamiwa na Liverpool. Walicheza kwa tahadhari kubwa huku wakipania kutorudia makosa yaliyochangia mabao waliyopokezwa na Liverpool katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliokamilika kwa 5-2 mnamo Disemba 2019 uwanjani Anfield.

Matokeo hayo ndiyo yalichangia kutimuliwa kwa mkufunzi Marco Silva ambaye nafasi yake ilitwaliwa na Ancelotti ambaye kwa sasa anakiandaa kikosi chake kupepetana na Norwich City mnamo Juni 24 uwanjani Carrow Road.