Habari Mseto

Kongamano la kikundi CSAK lafanyika MKU, suala la maadili kwa vijana lajadiliwa

May 30th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KWA minajili ya kuweka maadili mema miongoni mwa vijana nchini, kikundi cha Kikristo cha Christian and Scientific Association of Kenya (CSAK), kimebuniwa kuwa kielelezo cha maadili na tabia njema kwa vijana.

Mkurugenzi mkuu wa CSAK Profesa Francis Muregi aliyezindua mpango huo alisema huo ni mwelekeo wa kuonyesha “unyenyekevu wako kwa maswala ya kidini na kimaadili.”

Prof Muregi alisema vikundi vingine vya aina hiyo vitazinduliwa katika vyuo 40 vilivyo na uhusiano na CSAK.

Prof Francis Muregi (kushoto) akihudhuria kongamano la vijana la CSAK lililofanyika katika ukumbi wa Arena Indoors, Chuo Kikuu cha Mount Kenya mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tunataka kuweka msimamo wa kujielewa miongoni mwa vijana ili kujifunza jinsi ya kuelewana ama kutoelewana kwa njia ya mazungumzo,” alisema Prof Muregi.

Hafla hiyo iliandaliwa katika ukumbi wa Indoor Arena katika Chuo cha Mount Kenya mjini Thika na kuhudhuriwa na watu wa tabaka mbalimbali.

Alisema anaelewa vijana mara nyingi wanatofautiane kwa njia moja ama nyingine, kisiasa, kitamaduni na kisayansi lakini hayo hayastahili kusababisha kushambuliana kwa vita.

Alisema kikundi hicho kitapewa mafunzo mazito jinsi ya kushirikiana pamoja miongoni mwao bila kusababisha chuki huku wakihimizwa kuzuia hazira wanapokabiliana na maswala mazito.

Msomi Dkt Mohamed Mranja, ambaye ni mhadhiri mkuu kwa masomo ya Dini katika Chuo cha Moi, alisema Dini ya kiislamu hakiungi mkono uavyaji wa mimba, pengine tu mama mhusika akiwa na hatari ya kiafya.

Kwa hivyo aliwashauri wanafunzi wawe makini wanapojumuika na wenzao na wajue kujizuia mambo yanayoweza kudhuru maisha yao.

Profesa Joseph Galgalo wa Chuo cha St Paul’s mjini Limuru, alisema binadamu yeyote hana ruhusa kusitisha kiumbe cha Mungu kwa sababu ni dhambi mbele ya mwenyezi Mungu.

Alimsifu mwanzilishi wa Chuo cha Mount Kenya Profesa Simon Gicharu kwa kuunga mkono miradi mengi ambayo huendeshwa katika chuo hicho.

“Chuo hiki limepiga hatuo kubwa kutokana na hatua nzuri waliyochukua ya kuwapa wanafunzi nafasi ya kuonyesha ubunifu wao kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa,” alisema Prof Galgalo.

Profesa Elizabeth Bukusi, mtafiti katika kituo cha utafiti cha Kemri alisema uavyaji mimba hauruhusiwi hata kwa katiba na alipinga jambo hilo.

Mchungaji (Pastor), Reuben Kigane, alilaumu pendekezio lililotolewa juzi kuwa vijana wazima watambuliwe kutoka miaka 16 badala ya 18.

“Mawazo hayo hayawezi kukubalika hata kidogo kwa sababu hiyo ni njia ya kulipotosha kizazi kijacho bila kuwapa mwongozo ufaao,” alifafanua mchungaji Kigane.

Naibu Chansela wa Chuo cha Mount Kenya Profesa Stanely Waudo, alisema mkutano huo ulikuwa na umuhimu wake mkubwa kwa sababu kila mmoja amepata nafasi ya kujielewa kwa uwazi bila utata wowote.

“Ni vyema wakenya kuelewa maswala yote muhimu katika maisha yao, hasa kuhusu maisha kupitia mawazo ya kisayansi na dini. Lakini maswala ya kigeni kuhusu upangaji wa uzazi na utumizi wa dawa za uzazi unastahili kujadiliwa kwa uwazi ili kusije kuwa na utata wowote katika nchi yetu,” alisema Prof Waudo.