Habari za Kitaifa

Koome awateua majaji watatu kusikiliza kesi inayopinga sheria za afya

March 5th, 2024 1 min read

NA SAM KIPLAGAT

JAJI Mkuu Martha Koome ameteua jopo la majaji watatu ambao watasikiliza kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIA), ambayo serikali inalenga kuitumia ili kutimiza mpango wa Afya Bora kwa Wote (UHC).

Jaji Koome aliwateua majaji wa Mahakama Kuu Alfred Mabeya, Robert Limo na Dkt Freda Mugambi, kutoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasiliswa na Bw Joseph Enock Aura mwaka 2023.

Taasisi husika, likiwemo Bunge la Kitaifa, zilikuwa zimeirai mahakama kuwateua majaji watatu kuamua uhalali wa sheria hizo.

Taasisi zilisema kwamba kesi hiyo ilizua maswali muhimu, kwa mfano ikiwa kuna mfumo wa kisheria wa kusimania bima ya afya ya jamii nchini, baada ya kufutiliwa mbali kwa Bima ya Kitaifa ya Hospitali (NHIF).

Bw Aura anataka faili ya kesi hiyo kuwasilishwa mbele ya Jaji Mkuu Martha Koome, ili awateue majaji watatu kutoa uamuzi kuihusu.

Kesi hiyo itatajwa mbele ya majaji hao mnamo Machi 12, 2024.

“Kesi hiyo inazua masuala mazito ya kisheria, kuhusu utekelezaji wa Kipengele 31 cha Katiba, hasa kuhusu uwekaji data za watoto bila kibali chao na jamii,” akasema Bw Aura kupitia wakili wake, Bi Sandra Nganyi.

Mlalamishi anataka SHIA 2023, Sheria ya Afya ya Msingi 2023 na Sheria ya Afya Kidijitali 2023 kufutiliwa mbali, akisema kuwa zinakiuka Katiba.