Habari za Kaunti

Kuapishwa kwa Joho kwayeyusha Gen Z Lamu wakidinda kuandamana

Na KALUME KAZUNGU August 8th, 2024 2 min read

MABADILIKO ya Baraza la Mawaziri, hasa uteuzi wa Gavana wa zamani wa Mombasa, Bw Hassan Ali Joho kuwa Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini  yamepatia vijana wa Gen Z Kaunti ya Lamu  matumaini tele, na kuwafanya kudinda kushiriki maandamano ya Alhamisi, Agosti 8,2024, almaarufu ‘Nane Nane’.

Vijana hao waliozungumza na Taifa Leo Dijitali kisiwani Lamu,  walikiri kuwa wao kama jamii ya wavuvi na watega uchumi wa baharini,  wanahisi Rais William Ruto amewasikiliza na kutenda haki kwa kumteua Bw Joho.

Kulingana na vijana hao, Bw Joho ni mchapa kazi na mwenye tajiriba katika masuala ya baharini na kwamba wanaamini kuwa changamoto za jamii ya wavuvi, hasa Lamu na Pwani kwa jumla zitashughulikiwa na sekta kuboreshwa kikamilifu.

Mmoja wa vijana hao, Bw Mohamed Omar,  alieleza matumaini yake kwa Waziri Joho,  kwamba atafanya vyema kuimarisha yale ambayo mtangulizi wake katika wizara hiyo, Bw  Salim Mvurya alianzisha.

“Sioni sababu inayotufanya kuandamana barabarani leo. Tunahisi tumetosheka. Rais Ruto alihakikisha Wapwani kama vile Bw Joho na Bw Mvurya wapo kwenye baraza jipya. Kilichotuyeyusha moyo zaidi hivyo kutufanya kusitisha maandamano leo,  ni kumuona Bw Joho akiapishwa,” akasema Bw Omar.

Aliongeza, “Tuko na imani na matarajio makuu kwa Bw Joho kwamba atalainisha sekta ya Uchumi wa Baharini, ikizingatiwa kuwa Pwani, hasa Lamu ni jamii ya wavuvi. Tuwaacheni mawaziri wetu wapya wafanye kazi.”

Kijana mwingine aliyekataa kutaja jina lake,  alisema wao wametosheka na orodha ya mawaziri wapya walioteuliwa na kuapishwa na Rais Ruto Alhamisi,  Agosti 8, 2024.

Alisisitiza kwamba uteuzi wa Bw Joho kwenye sekta ya Madini na Uchumi wa Baharini ndicho kichocheo kikuu kilichopelekea wao kusitisha maandamano.

“Twahisi Waziri Joho ni kipenzi chetu, kijana sharobaro mwenzetu na mchapa kazi. Kinachotufanya kuweka matumaini zaidi kwa Bw Joho ni kuona ameboresha chuo wa ubaharia kilichozinduliwa hapa Lamu. Pia ahakikishe ajira zinapatikana, kupanuka na pia elimu ya Uchumi wa Baharini  ipewe kipaumbele, hasa kwenye taasisi zetu anuwai (TVETs),” akasema kijana huyo.

Vijana hao pia walimpongeza Rais Ruto kwa uteuzi wa  aliyekuwa gavana  Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, Mbunge wa zamani wa Suba Kusini, John Mbadi na Kiongozi wa Wachache Bungeni, Bw Opiyo Wandayi na wengineo, wanajumuishwa kwenye baraza jipya la mawaziri.

“Tuko sawa kuona viongozi ngangari wa upinzani wamejumuishwa kwenye baraza la mawaziri. Yaani hilo baraza jipya ni la wachapa kazi tu,” akasema kijana mwingine.

Wakati huo huo, shughuli za kawaida, ikiwemo biashara na uchukuzi ziliendelea bila kutatizwa kwenye miji yote mikuu ya Lamu Alhamisi.

Hii ni licha ya sehemu zingine za nchi kama vile Nairobi kushuhudia taharuki iliyopelekea sehemu za kibiashara, ikiwemo maduka kusalia kufungwa kutokana na maandamano ya Nane Nane.

Taifa Leo ilitembelea Mji wa Kale wa Lamu, Shella, Mokowe, Hindi, Mpeketoni, Hongwe, Baharini, Kibaoni, Majembeni na Witu, ambapo hali ilikuwa  shwari na tulivu.

“Sisi hapa ni kazi tu. Hatufahamu maandamano eti ya Nane Nane. Pengine hayo maandamano na ghasia ni Nairobi na kwingineko. Hapa Lamu sisi ni kujenga taifa tu,” akasema Bw Japheth Kariuki ambaye anafanya kazi za ujenzi.