Habari za Kitaifa

‘KUPUMZIKA NI MBINGUNI’: Kawira matatani kwa mara ya tano

Na DAVID MUCHUI August 1st, 2024 2 min read

UHASAMA wa kisiasa katika Kaunti ya Meru ulitokota zaidi Jumatano baada ya diwani kuwasilisha hoja ya tano ya kumtimua Gavana Kawira Mwangaza uongozini.

Hoja hiyo iliwasilishwa katika bunge la kaunti na diwani mteule Zipporah Kinya. Hii ilikuwa hoja ya tano baada ya ile ya nne kuwasilishwa mnamo Jumanne.

Aidha hoja ya Jumatano iliwasilishwa siku mbili baada ya Bi Mwangaza kupata afueni kufuatia mahakama kuamua mzozo kati yake na madiwani uwasilishwe kwa Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke.

Bi Kinya, ambaye ni Naibu Kiongozi wa Wengi Bunge la Kaunti ndiye aliondoa hoja ya kumtimua Bi Mwangaza mnamo Jumanne katika kile kilichoonekana kukwepa mitego au vizingiti vya kisheria.

Katika hoja ya Jumatano, Bi Kinya alisema kuwa gavana huyo anastahili kuondolewa afisini kwa kukiuka katiba na pia matumizi mabaya ya afisi.

“Kuendelea kukaa kwake afisini kumetia doa utoaji wa huduma na kulemaza matarajio ya wakazi wa kaunti,” akasema Bi Kinya.

Baada ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo, Bi Mwangaza aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa ana matumaini atatatamba kwa mara nyingine baada ya majaribio ya nyuma ya kumbandua kufeli.

“Hoja hiyo imekufa hata kabla haijajadiliwa,” akasema Bi Mwangaza.

Wakili wa Gavana Mwangaza, Bw Elias Mutuma alionya bunge la kaunti dhidi ya kuwasilisha mswada huo akisema ni kukiuka amri korti. Hata hivyo, wakili wa bunge la kaunti Ndegwa Njiru alisema hakukuwa na amri yoyote inayoizua kaunti kuwasilisha hoja mpya ya kumtimua gavana.

Katika hoja mpya baadhi ya masuala ambayo yalikuwa katika hoja ya mwanzo yameondolewa. Kati ya masuala hayo ni kutimuliwa kwa mshauri wa masuala ya kisheria wa gavana na pia kuajiriwa kwa mwanasheria mkuu wa kaunti bila idhini ya bunge la kaunti.

Diwani huyo amesema gavana alikiuka sheria kwa kubatilisha uteuzi wa Katibu wa Bodi ya Kaunti Virginia Kawira, kukataa kuwateua wanaoshikilia uenyekiti wa bodi mbalimbali na kukataa kutekeleza mapendekezo ya kaunti.

Makosa mengine ni kuwatimua wakuu wa bodi na kuhadaa umma kutokana na kudai kuwa madiwani walikuwa wamechangisha Sh86 milioni kwa familia ya bloga marehemu Bernard Muthiani maarufu kama Sniper.

Pia Bi Mwangaza amelaumiwa kwa kulipa bila kufuata sheria Sh74.3 milioni kama marupurupu kwa madaktari, kuwaajiri wafanyakazi 111 ambao wanahudumu kwenye afisi yake. Kuajiriwa kwa wafanyakazi hao kulichangia gharama ya kaunti kupanda kwa Sh500 milioni kisha Sh103 milioni kulipwa nje ya mfumo wa kawaida wa ulipaji mshahara.

Kama hayo hayatoshi gavana amelaumiwa kwa kulipa Afisa wa Mawasiliano Christus Manyara mshahara ilhali alikuwa ameshtakiwa kwa mauaji, kulipwa kwake kukienda kinyume na mwongozo wa ulipaji wa watumishi wa umma.

Mahakama ilikuwa imeamrisha mzozo kati ya gavana utatuliwe na Njuri Ncheke lakini baraza hilo la wazee likajiondoa. Kamati iliyoteuliwa na Rais William Ruto kusikiza pande zote mbili kisha kuwasilisha ripoti yake imesema kuwa ishaandaa ripoti yake na inasubiri tu miadi na rais ili kuiwasilisha