Habari za Kitaifa

KUSOTA NI WEWE: Jinsi utajiri wa mawaziri ulivyoongezeka kwa zaidi ya Sh100M miaka miwili

Na MARY WANGARI August 2nd, 2024 2 min read

MAWAZIRI watatu wateule wamefichua jinsi thamani ya utajiri wao ilivyoongezeka kwa mamilioni katika kipindi cha miaka miwili walipokuwa wakihudumu kabla ya Rais William Ruto kuwapiga kalamu.

Profesa Kithure Kindiki na Bi Alice Wahome waliobahatika kupatiwa fursa ya pili kuhudumu tena kama mawaziri wa usalama wa ndani na ardhi, mtawalia, katika baraza jipya, wamekiri kuwa utajiri wao uliongezeka kwa zaidi ya Sh100 milioni.

Kamati Maalum ya Bunge la Kitaifa ilisikia Alhamisi kuwa utajiri wa Profesa Kindiki uliongezeka kwa Sh150 milioni hadi kufikia Sh695 tangu alipochukua usukani kama waziri wa usalama wa ndani.

Hata hivyo, Profesa Kindiki, akipigwa msasa na kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, alikanusha kuwa utajiri wake umeongezeka kutokana na shughuli haramu.

“Jinsi nilivyosema nilipohojiwa mara ya kwanza, utajiri wangu ulikuwa Sh544 milioni kabla ya uteuzi wangu. Sasa umeongezeka hadi Sh694 milioni,” alisema Profesa Kindiki.

“Sijanufaika kutokana na biashara yoyote haramu na sijawahi kufanya biashara yoyote na serikali.”

Aidha, Profesa Kindiki anayemiliki shirika la mawakili alikana kwamba utajiri wake umeongezeka kutokana na mshahara au malimbikizi aliyokuwa akipata kama waziri.

“Ingawa kwa sasa sihudumu kama wakili, shirika langu la sheria lingali hai na linafanya kazi,” alisema.

“Mshahara wangu wote unatumika kulipa bili.”

Bw Kindiki vilevile alifichua kuwa deni alilolipwa miezi miwili tu baada ya kuteuliwa kama waziri kwa mara ya kwanza, lilichangia kuongeza mali yake.

Kando na Shirika lake la mawakili, Bw Kindiki alisema kuwa anamiliki biashara ndogondogo akisisitiza kuwa, “hakuna utajiri wangu umetokana na mshahara au malimbikizi.”

Alisema jumla mali anayomiliki inajumuisha majumba mawili yenye thamani ya Sh235 yaliyopo jijini Nairobi na Tharaka Nithi, magari yenye thamani ya Sh17 milioni, akiba katika mashirika ya Sacco na mapato kutokana na shirika lake la mawakili.

Kwa upande wake Bi Wahome, alisema thamani ya utajiri wake, unaojumuisha mali yake pamoja na mume wake, iliongezeka kwa Sh103 milioni hadi kufikia Sh327 milioni kutoka Sh224 milioni katika muda wa miaka miwili alipoongoza Wizara ya Ardhi.

“Utajiri wangu umeongezeka kutokana na kuimarika kwa sekta ya ustawishaji na malipo ya malimbikizi ya kodi,” alifafanua Bi Wahome.

Waziri mteule kwa wizara ya ulinzi, Bi Soipan Tuya, alisema kuwa thamani ya utajiri wake iliongezeka hadi Sh243.4 milioni kutoka Sh156 milioni alipochukua usukani kama waziri wa mazingira miaka miwili iliyopita.

Wengine waliotangaza thamani ya utajiri wao ni pamoja na Bi Debora Barasa, waziri mteule wa afya aliyefichua kuwa thamani ya mali anayomiliki pamoja na mume wake ni Sh455 milioni.

Bw Julius Migos, waziri mteule anayetazamiwa kumrithi aliyekuwa waziri wa elimu, Ezekiel Machogu, alitangaza vilevile utajiri wake kiasi cha Sh790 milioni.