Habari za Kitaifa

Kwa nini wabunge wa ODM walisusia mwaliko Ikulu?

Na MOSES NYAMORI September 11th, 2024 2 min read

MGAWANYIKO kuhusu ushirikiano kati ya ODM na Kenya Kwanza unaendelea kudhihirika.

Hali hii inatajwa kuwa sababu kuu ya wabunge wa chama hicho kususia mkutano wa Rais William Ruto katika Kaunti ya Nairobi mnamo Jumatatu.

Rais Ruto alikuwa mtaani Kibera akikagua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, hafla ambayo wabunge wote wa ODM walialikwa lakini baadhi wakasusia.

Kenya Kwanza na ODM zilianza ushirikiano wakati maandamano ya Gen Z yalifika kilele chake nchini. Hatua hiyo ilisababisha viongozi wakuu wa ODM kuteuliwa mawaziri serikalini.

Hata hivyo, tofauti zilizoibuka baada ya ushirikiano huo kukumbatiwa ulidhihirika wabunge walipokosa kuandamana na Rais mtaani Kibera na kususia mkutano aliokuwa ameitisha nao katika ikulu ya Nairobi.

“Hujambo, natumai umeamka vizuri kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Kwa dharura na pole kwa notisi ambayo imekuja kwa muda mfupi. Rais ameomba tuandamane naye wadi ya Highrise, eneobunge la Langáta saa 11 asubuhi kukagua ujenzi wa nyumba,” ukasema ujumbe kutoka kwa Mbunge wa Makadara George Aladwa

“Sisi kama wabunge wa ODM Kaunti ya Nairobi tutakuwa na kikao na Rais katika ikulu ya Nairobi baada ya hafla hiyo,”ukaongeza ujumbe huo wa Bw Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi.

Ni Bw Aladwa, Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi, Phelix Odiwuor maarufu kama Jalango (Langata) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris waliohudhuria hafla ya Kibera na kisha kukutana na kiongozi wa nchi katika ikulu ya Nairobi.

Seneta Edwin Sifuna ambaye pia ni Katibu wa ODM, wabunge Anthoy Oluoch (Mathare), Peter Orero (Kibra), Babu Owino (Embakasi Mashariki), Tom Kajwang’ (Ruaraka) na Tim Wanyonyi hawakuhudhuria.

Bw Sifuna alisema kuwa Rais angetambua kuwa kuna mamlaka tofauti kati ya Afisi ya Rais na Bunge. Aliongeza kuwa kiongozi huyo wa UDA hana mamlaka ya kuagiza wabunge wa ODM wafike mkutano wake.

“Mwanzo, Rais hana mamlaka ya kuitisha mkutano na wanachama wa ODM. Pili kama seneta, ni ukiukaji mkubwa wa katiba ambayo imetenga mamlaka kwa Rais kutualika ikulu,” akasema Bw Sifuna

“Mwaliko huo haukuwa wa heshima na ulikuwa unalenga kumpiga jeki kisiasa,” akaongeza.

Bw Owino naye alisema kuwa atakutana na Rais Ruto wakati ambapo serikali yake itatimiza ahadi yake kwa Wakenya. Bw Owino ni kati ya wabunge wa ODM ambao bado hawajachangamkia ushirikiano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga.

Azma ya Bw Odinga ya kuendea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ilipokuwa ikizinduliwa ikulu wiki mbili zilizopita, Bw Owino alikuwa kwenye kikao na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Bw Musyoka kwenye kikao hicho alikuwa akijitangaza kiongozi wa upinzani kutoka kwa Bw Odinga ambaye amejiondoa katika siasa za Kenya.

“Hzuwezi kuwa pande zote na mimi naegemea mrengo wa raia kwa sababu Ruto hafanyi chochote kwa Wakenya. Akianza kutimiza ahadi zake ndipo nitaketi naye lakini kwa sasa sina chochote cha kujadili naye,” akasema Bw Owino.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye alihudhuria hafla zote mbili alisema kuwa wabunge walikosa kuhudhuria kwa sababu walitumiwa mwaliko kuchelewa na wale waliokwepo ndio walihudhuria.

Bw Sakaja alisema kuwa Serikali Jumuishi kwa sasa inaunganisha viongozi wote wa Nairobi. Alisema kuwa mipango inaendelea ili viongozi wote waliochaguliwa Nairobi wakutane na Rais ikuluni.

“Tumeona Rais akiongea na viongozi wa kaunti nyinginezo kabla ya kuanza ziara ya maendeleo na tunahisi Nairobi haistahili kuachwa nyuma,” akasema Bw Sakaja.

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ODM Jumatatu alieleza Taifa Leo kuwa kwa sasa chama kimegawanyika na hawajui wachukue mwelekeo wa kupinga au kuunga serikali