Michezo

Leteni hao majeruhi Bayern tuwape dozi, Arsenal sasa yajigamba

April 9th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

KIUNGO mshambuliaji Martin Ødegaard amesema Arsenal hawaogopi vigogo wa Ujerumani, Bayern Munich anayochezea straika matata Harry Kane, timu hizo zitakapotifua kivumbi katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Emirates Jumanne usiku.

Ushindi shadidi dhidi ya wenyeji Brighton kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ulikuwa wa 10 kati ya 11 zilizopita ligini tangu mwaka huu uanze.

Isitoshe, timu hiyo maarufu The Gunners imefunga magoli 38 na kufungwa manne pekee tangu Januari.

Matokeo ya Jumamosi yalipaisha masogora wa kocha Mikel Arteta hadi kileleni mwa EPL na alama 71.

“Tunaheshimu (Kane na Bayern yake) lakini hatufai kuogopa yeyote. Letu ni kuangalia ubora wetu. Ni mchezaji mzuri, nimecheza dhidi yake mara kadhaa na ninajua ubora wake hususan katika kijisanduku,” alisema Ødegaard kuelekea robo-fainali ya leo, ambayo Gunners wanashiriki awamu hii kwa mara ya kwanza tangu 2010.

Nahodha huyo wa Arsenal alipoulizwa iwapo timu iko tayari kukabili vigogo wa kocha Thomas Tuchel alihoji: “Kila mechi ina changamoto zake. Bayern ni timu nzuri yenye wachezaji mahiri hususan katika mashambulizi.

“Wamekuwa na fomu zegezege ligini (Bundesliga). Lakini tunajua ni timu mahiri yenye wachezaji wa nguvu. Hivyo, utakuwa usiku wa fataki uwanjani Emirates, lakini tuko tayari!”

Fomu hobelahobela

Bayern imekumbwa na matokeo duni katika Bundesliga (Ligi Kuu ya Ujerumani) na kufuatia kichapo cha 3-2 mikononi mwa wenyeji Heidenheim wikendi na ni wazi hawatatetea ubingwa wao.

Vinara Bayer Leverkusen, ambao hawajapoteza mechi msimu huu, wana pointi 76 baada ya ushindi wikendi — alama 16 zaidi ya Bayern zikisalia mechi tatu ligi hiyo ya timu 18 ifike tamati.

Leverkusen watatawazwa mabingwa wa Bundesliga iwapo watashinda mechi ya wikendi ijayo.

Licha ya fomu yao duni, Bayern wamekuwa mwiba kwa Arsenal katika mechi za kombe la UEFA.

Wajerumani hao wamelima Arsenal mechi tatu zilizopita 5-1.

Baada ya kuwalemea katika mechi za makundi msimu 2015-16, Bayern iliwagaragaza kwa jumla ya magoli 10-2 katika awamu ya 16-bora msimu uliofuata 2016-2017 na kuwa kichapo kibaya zaidi kwa Arsenal mikononi mwa wauaji wao hao gozi la bara Ulaya.

Kitawaka pia Bernabeu

Katika robo-fainali ya pili leo, mabingwa watetezi Manchester City watakuwa wageni wa Real Madrid katika uwanja wa Santiago Bernabeu.

Timu hizi zimekutana mara 10 katika Klabu Bingwa Real ikipata ushindi mara tatu nao Man-City wakiwika mara nne. Zimetoshana nguvu katika mechi tatu.

Man-City walishinda taji hilo mwaka jana – lao la kwanza kabisa la UEFA.

“Ni mchuano wa kuvutia katika ulimwengu wa soka. Sitaki kusema itakuwa kama msimu uliopita, kwa sababu kila mchuano una sifa zake. Tuone nini kitatokea baada ya dakika 180,” alisema kocha wa Real, Carlo Ancelotti.

Mwenzake wa Man-City, Pep Guardiola, akishikilia uzi huo huo wa ushindani mkali aliongezea: “Ni timu tofauti kabisa na msimu uliopita. Kukabili Real Madrid ni changamoto kubwa daima. Ni klabu ya kipekee na katika mashindano haya wanaweza kudhibiti mambo mengi kwa uzoefu walionao.”

Real Madrid ndio baba lao UEFA kwani wanashikilia rekodi ya kunyanyua kombe hilo mara nyingi zaidi – 14 – ikiwemo misimu mitatu mfululizo (2016, 2017 na 2018).

AC Milan ndio wa pili katika orodha hiyo na mataji saba kisha Liverpool wanafunga tatu-bora na mataji sita.