Habari za Kitaifa

LSK yaishtaki serikali kuhusu usambazaji wa My-Gov

February 17th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha Mawakili Nchini (LSK) kinaomba Mahakama Kuu ifutilie mbali agizo matangazo yote ya serikali yachapishwe katika gazeti la The Star linalomilikiwa na Radio Africa Group.

Katika kesi iliyoshtakiwa katika mahakama ya Milimani, LSK inasema agizo la Katibu wa Wizara ya Masuala ya Teknolojia Edward Kisiang’ani kwamba matangazo yote ya Serikali, mashirika ya serikali, vyuo vikuu na mashirika huru yawe yakitangaza habari zao katika Gazeti la The Star inakiuka haki.

Prof Kisiang’ani alitoa agizo hilo mnamo Januari 23, 2024.

Katika barua aliyowaandikia makatibu wakuu na vinara wa asasi za serikali, Prof Kisiang’ani aliamuru matangazo yote yachapishwe na Convergence Media na Star Publications Limited.

“Agizo hili ni ukiukaji wa sheria na mwongozo wa serikali kwamba habari muhimu za serikali zipashwe umma na magazeti yanayosomwa kusambazwa kote nchini,” afisa mkuu wa LSK Bi Florence Muturi amedokeza katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama kuu Milimani.

LSK inasema kwamba serikali huchapisha matangazo yake katika jarida la My-Gov kwa lengo la kuwapasha Wakenya wote habari muhimu, mwongozo wa serikali, kusaka utoaji wa huduma kwa umma, kusaka ajira kwa serikali na utoaji wa huduma nyingine muhimu za serikali.

Jarida hilo la Serikali lilikuwa likisambazwa na magazeti manne ya humu nchini ambayo ni Daily Nation, The Standard, The Star, na The People Daily. Kandarasi ya kusambaza jarida hili la My-Gov iliisha Desemba 2023.

Baada ya kandarasi hii kukamilika muda wake, serikali iliweka matangazo kualika kampuni za magazeti kusambaza My-Gov.

Badala ya serikali kusubiri kampuni zenye uwezo kusambaza My-Gov kushiriki, iliteua The Star kinyume cha sheria, inasema LSK.

LSK inasema waziwazi kwamba The Star sio Gazeti linalosambazwa kote nchini bali lina soko kubwa jijini Nairobi.

Hii inamaanisha jarida la My-Gov  litatakuwa linasambazwa Nairobi tu.

Bi Muturi alisema Serikali haikufanya mashauri ya kutosha na washika dau ama kuwahoji Wakenya wanaopokea huduma zake kabla ya kuiteua The Star kusambaza My-Gov.

Wakili huyu ameeleza mahakama kwamba Serikali haikushirikisha umma na kupata maoni ya umma kabla ya kuipa The Star kandarasi hiyo.

“Serikali ilichukua hatua hii kabla ya kufanya mahojiano na umma na washika dau kulingana na  Vifungu vya Katiba nambari 10(2) na 201,” asema Bi Muturi katika kesi aliyowasilishwa kwa sheria za dharura.

Alisema serikali imekaidi sheria kupitia uteuzi wa The Star kusambaza My-Gov na kuomba mahakama kuu ifutilie mbali uamuzi huo.

“Kuteua The Star kusambaza My-Gov, serikali imepotoka na kukaidi sheria na uhuru wa vyombo vya utangazaji kielektroniki, magazeti na aina nyingine za usamabazaji habari. Sheria imepinga serikali kutamalaki usambazaji wa habari kupitia njia yoyote ile,” asema Bi Muturi.

LSK imesema kwamba serikali ilibagua kampuni nyingine ilipoteua The Star.

Pia LSK imesema serikali imekaidi kifungu nambari 35 (3) kinachosema usambazaji wa habari kwa umma utekelezwe na kampuni iliyo na uwezo wa kuwafikia watu wengi.

LSK imesema Prof Kisiang’ani hana mamlaka kuwapa maagizo wakuu wengine wa mashirika na asasi za serikali.