Habari za Kaunti

Maafisa wa kanjo kupewa mafunzo na KFS kujua kuishi na raia  

January 21st, 2024 1 min read

NA GEORGE ODIWUOR

SERIKALI ya Kaunti ya Homa Bay imeanzisha mafunzo kwa maafisa wake wa usalama ‘kanjo’ ili kuhakikisha kuwa wana nidhamu wanapotekeleza wajibu wao.

Mafunzo hayo yatakuwa yakiendeshwa na maafisa wa Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS) kwenye akademia yao ya mafunzo Londiani, Kaunti ya Kericho.

Kaunti inasisitiza kuwa mafunzo hayo yatahakikisha kuwa maafisa hao wa usalama wapo fiti wanapotekeleza wajibu wao.

Watakaopita vizuri mafunzo hayo wataanza pia kufahamishwa kuhusu masuala ya mengine ambayo wanastahili kuzingatia wakiwa kazini.

Kundi la maafisa 250; wakiwemo wanawake 48 wameteuliwa kushiriki mafunzo hayo ambayo yatachukua muda wa mwezi moja.

Wengine waliosalia nao watapokea mafunzo hayo muhimu katika mwaka ujao wa fedha.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari-mseto/wafanyakazi-hewa-waliotimuliwa-na-gavana-wanga-wapata-mtetezi

Kumekuwa na uhasama mkubwa kati ya wafanyabiashara na maafisa wa usalama ambao huwa ni wakali na huwachapa baada ya kuwakamata.

Baada ya mafunzo hayo, maafisa hao wa usalama wanatarajiwa kuwa na urafiki na raia na kubadilisha mtazamo hasi ambao raia wamekuwa nao dhidi yao.

Waziri wa Ugatuzi katika kauti hiyo Mercy Osewe alisema kuwa ‘kanjo’ hao watakuwa na mtindo mpya wa uchapakazi baada ya mafunzo hayo na watasuluhisha utata wowote kwa njia ya uungwana.

“Mafunzo hayo ni bora kwa utendakazi wao wa kibinafsi, kisaikolojia na kikazi. Ujuzi huo ni muhimu kuhakikisha kuwa wanashughulikia raia kwa njia ya utaalamu,” Bi Osewe akasema.