Afya na JamiiMakala

Maambukizi ya HIV ni tishio kwa vijana wa Homa Bay

Na PAULINE ONGAJI September 20th, 2024 3 min read

TANGU utotoni ndoto yake Bi Achieng (sio jina lake), 24, ilikuwa kujiendeleza kimaisha.

Kwa hivyo, Bi Achieng, mkazi wa eneo la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, alifanya kila jitihada kufanya vyema shuleni angalau kupata nafasi chuoni na kusomea mojawapo ya taaluma alizoenzi: udaktari, uhandisi au urubani.

Lakini Novemba 2020, wakati huo akiwa na miaka 20, ndoto yake ilionekana kufikia kikomo alipogundua kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi: HIV.

“Katika shughuli zangu za kawaida jijini nilipita karibu na kituo cha VCT ambapo wahudumu walinishawishi nifanyiwe uchunguzi kujua hali yangu ya HIV,” aeleza.

Kulingana na Bi Achieng, alipigwa na butwaa matokeo yalipoonyesha kwamba alikuwa na virusi, hivi.

“Sikuamini ambapo nilidhani kwamba uchunguzi huo ulikuwa na makosa,” asema, huku akiongeza kwamba alilazimika kufanyiwa chunguzi zingine kadhaa tofauti ambapo zote zilithibitisha matokeo ya awali.

Kwa mwaka mmoja hakukubali hali yake huku akijaribu kutafakari ni wapi na lini alipoambukizwa virusi hivi?

“Mawazo yote yalinielekeza kwa mwajiri wangu wa zamani ambapo baada ya kufanya uchunguzi niligundua kwamba alikuwa amefariki miezi kadhaa iliyopita baada ya kuugua maradhi ambayo sikufichuliwa, huku nikielezwa kwamba alikuwa amekataa kupokea matibabu,” aeleza.

Kwa hivyo ni vipi mawazo yake yalimwelekeza huko? Kutokana na sababu kuwa Bi Achieng alikuwa akitoka katika familia maskini, wazazi wake walikuwa na matatizo ya kumpeleka shuleni pamoja na nduguze.

“Nilipokuwa katika shule ya upili ilikuwa ngumu kupata karo, na hivyo wakati mwingi ningekaa nyumbani kutokana na ukosefu wa karo. Nililazimika kuacha shule na kutafuta ajira.”

Kwa hivyo alisafiri kutoka mashambani hadi mjini Homa Bay ili kusaka ajira. “Sikuwa na pesa wala fursa yoyote nilipowasili jijini.”

Kwa bahati nzuri, hatimaye alipata kazi kama mjakazi. Siku zilivyozidi kusonga, uhusiano kati yake na mwajiri wake ulinawiri, suala lililomsababisha kualikwa na kupewa chumba cha kulala nyumbani mwa mwajiri wake.

“Siku moja aliniahidi kunirejesha shuleni iwapo ningekubali kushiriki naye tendo la ndoa naye bila kinga, ombi ambalo nilitimiza,” asema.

Hata hivyo baadaye ahadi ya kurejeshwa shuleni iligonga mwamba kwani mwajiri wake alipoteza ajira, na hivyo kumfurusha huku akidai kwamba hakuwa na pesa za kuendelea kumlipa.

Bi Achieng anawakilisha idadi inayozidi kuongezeka ya vijana kutoka eneo hili ambao wameambukizwa virusi vya HIV katika eneo hili kabla ya kutimu miaka 25.

Japo utafiti unaonyesha kwamba Kaunti ya Homa Bay imepiga hatua katika kupambana na maambukizi ya virusi hivi, bado sehemu hii inabeba mzigo mkubwa wa maambukizi ya virusi hivi.

Takwimu kutoka kwa mpango wa kitaifa wa kudhibiti maambukizi ya ukimwi na magonjwa ya zinaa (NASCOP), unaonyesha kwamba kaunti ya Homa Bay inaongoza katika via vya maambukizi ya maradhi haya. Aidha, utafiti mwingine unaonyesha kwamba maambukizi ya virusi vya HIV katika Kaunti ya Homa Bay ni asilimia 26.0, kiwango ambacho ni takriban mara 4.5 zaidi ya viwango vya maambukizi kitaifa. Aidha, kaunti hiyo ilichangia asilimia 15.1 na asilimia 14.0 ya maambukizi mapya miongoni mwa watoto na watu wakomavu respectively, nchini Kenya.

Kitaifa, vijana ndio wanaobeba mzigo mkubwa  wa maradhi haya. Utafiti wa Baraza la kitaifa la kudhibiti ukimwi NACC kudadisi viwango vya maambukizi ya virusi vya HIV unaonyesha kwamba idadi ya vijana kati ya miaka 15 na24 wanaoambukizwa maradhi haya imekuwa ikiongezeka.

Kulingana na uchanganuzi huo uliotangazwa majuma machache yaliyopita, kati ya watu watano wazima wanaoambukizwa virusi vya HIV, wawili ni vijana kati ya miaka 15 na 24, ambapo idadi hii inawakilisha asilimia 40 ya maambukizi.

Aidha, vijana katika mabano haya kiumri waliwakilisha asilimia 10 ya vifo vyote vilivyosababishwa na maradhi ya Ukimwi.

Kulingana na Bw Job Akuno, mtaalam  wa mpango wa afya ya uzazi ya vijana, vijana wanaanza kujihusisha na masuala ya mapenzi mapema maishani, suala linalowaweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa.

Pia, Bw Akuno anahusisha shida hii na umaskini ambapo ukosefu wa ajira umewalazimisha vijana wengi kujiingiza katika mahusiano na watu waliowazidi kiumri kama mbinu ya kupata pesa na hivyo kujikimu.

Kwa upande mwingine, Shirika la Afya Duniani WHO, katika eneo hili, wasichana ndio wamo katika hatari kubwa hata zaidi ya maambukizi, huku wataalam wakihusisha janga hili na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Utafiti wa mwaka wa 2020 ulioagizwa na Kaunti ya Homa Bay na kufanywa na taasisi ya Overseas Development Institute, ikishirikiana na shirika lisilo la kiserikali linalohusika na masuala ya huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV nchini, LVCT Health, kwa ufadhili wa UNICEF, aidha unaonyesha kwamba tatizo la kufikia huduma za afya, vile vile umaskini vimechangia tatizo hili katika eneo kaunti hiyo.

Vivile utafiti huu ulionyesha kwamba kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia pia ni tatizo, huku wasichana wakiwa katika hatari zaidi ya maambukizi.

“Utapata kwamba wasichana wengi katika eneo hili wanaishi katika umaskini, suala linalofanya iwe changamoto kwao hata kufikia bidhaa za hedhi. Hii inawalazimu kujihusisha katika mapenzi mapema na watu waliowazidi umri, na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi ya virusi hivi,” aeleza Bw Akuno.

Kulingana na wataalam, ili kukabiliana na tatizo hili, itakuwa muhimu kukabiliana na tatizo la umaskini, vile vile kuhakikisha kwamba wasichana wanapata bidhaa za hedhi, na kuwepo kwa uhamasisho kuhusiana na maambukizi ya virusi hivi.

[email protected]