Habari Mseto

Machogu aanza juhudi za kuwapatanisha Arati na Osoro

January 13th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu ameelezea kufadhahishwa kwake na mgogoro wa kisiasa unaoendelea baina ya Gavana wa Kisii Simba Arati na mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro.

Kwa kuwa uhasama huo umeanza kuweka maisha ya watu wa eneo hilo hatarini, waziri Machogu ameanzisha juhudi za kupatanisha wawili hao kupitia viongozi wa makanisa.

Katika barua aliyowaandikia wawili hao Ijumaa, ambayo Taifa Leo ilifanikiwa kuiona, Bw Machogu alitaja ghasia zinazoendelea Kisii kama ‘za kutatanisha na kusumbua’ na kuongeza kuwa zinadumaza ustawi na utulivu ambao jamii ya Abagusii imeishi nao kwa miaka mingi.

“Ili kupata undani wa suala hilo, nimeamua kuwa mashauriano yaanzishwe kati ya viongozi ili hawa kutafuta suluhu ya hali hii isiyokubalika inayotishia kuchafua jina zuri la eneo letu ambalo halina amani tena,” waziri Machogu alisema.

Ili kumsaidia kuwazungumzia mahasimu hao, Bw Machogu, ambaye ndiye kiongozi wa hadhi kuu kutoka jamii ya Abagusii serikalini, atawahusisha askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kisii Joseph Mairura, Mhubiri Dkt Leonard Aencha wa dhehebu la Kiadventista (SDA) na Mhubiri Dkt Moses Mogita wa makanisa ya kiroho.

Vikao vya kwanza vya mashauriano hayo vinatarajiwa kuandaliwa Januari 17, 2024.

Wakili Mkuu wa Serikali Shadrack Mose pia amealikwa kwenye mashauriano hayo.

Hatua ya Machogu kuingilia kati mzozo kati ya wawili hao imekuwa ikitolewa na viongozi wengine kila mara akiwemo seneta Richard Onyonka.

Baadhi ya viongozi kutoka Kisii na wazee wa jamii wamekuwa wakisema hawajawahi kushuhudia siasa chafu kama za sasa katika eneo hilo hata tangu kustaafu kwa aliyekuwa kinara wa siasa za eneo hilo marehemu Simeon Nyachae.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Abagusii Araka Matundura, ni mmoja wa wadau ambao wametoa wito wa viongozi kushauriana na kuzika tofauti zao.

Bw Araka alionyesha kusikitishwa kwake na ghasia kama za Jumatatu wiki jana ambapo kulikuwa na ufyatulianaji risasi Katika eneobunge la Mugirango Kusini.

Ghasia hizo ziliwaacha watu wanne na majeraha mabaya ya risasi ilhali magari mengi yalipasukuwa vioo.

Katika kisa kingine cha mwezi Juni 2023, katika wadi ya Boikang’a Mugirango Kusini bado, Arati na Osoro walifarakana kupelekea wafuasi wa viongozi hao kuanza kupigana kwa mishale na mikuki.

Mwaka 2021, katika mazishi ya babake aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, Osoro (UDA) na Arati (ODM) walilimana ngumi mbele ya vinara wao Rais William Ruto na Raila Odinga kujaribu “kuwafurahisha”.

Kufuatia purukushani za hivi punde za ufyatulianaji risasi, chama cha ODM kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna kilielezea hofu zake kwamba maisha ya gavana Simba Arati yalikuwa hatarini.

ODM kilimtaka Osoro ambayo pia ni Kiranja wa Wengi Bungeni kuandikisha taarifa kuhusu anachokijua kuhusiana na ghasia za hivi majuzi jinsi alivyofanya Arati.

Mbunge huyo wa awamu ya pili hata hivyo amekana madai hayo.

Macho yote sasa yataangazia mashauriano hayo yatakayoongozwa na waziri Machogu kuona ikiwa yatazalisha matunda yoyote.