Habari Mseto

Madereva waliokwepa ushuru wakamatwa mpakani

August 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Madereva wa malori matatu waliokamatwa katika mpaka wa Kenya na Somalia kwa kukwepa ushuru wa Sh2 milioni walishtakiwa katika mahakama moja ya Wajir Alhamisi.

Watatu hao Shukri Mohamed Elmi, Mohamed Abdi Ahmed na Omar Ibrahim walishtakiwa kwa kukwepa ushuru kinyume na sheria inayosimamia forodha.

Malori hayo yalikamatwa na maafisa wa forodhani wa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA) saa chache kabla ya sikukuu ya Idd-Ul-Adha.

Miongoni mwa bidhaa zilizokamatwa ni magunia 1,584 ya sukari ya kikahawia kutoka Brazil, katoni 30 za maziwa ya unga kutoka Denmark na katuni 30 za mafuta ya kupika kutoka Malaysia, zote za thamani ya Sh 2 milioni.

Bidhaa hizo hazikuwa na stempu ya Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) kama inavyohitajika na sheria.

Walikamatwa baada ya maafisa hao kudokezewa na umma, baada ya kuonekana wakipandisha bidhaa hizo kwenye malori upande wa Somalia.