Habari za Kaunti

Magavana 6 wa Pwani wavuna minofu katika ziara yao Italia

Na WINNIE ATIENO July 18th, 2024 2 min read

ZIARA ya magavana sita wa Pwani nchini Italia imewavunia wawekezaji wa kimataifa ambao watakita kambi nchini Kenya mwezi ujao.

Gavana wa Kilifi Bw Gideon Mung’aro, alisema ziara yao rasmi iliyoanza wiki iliyopita, tayari imesaidia kupiga jeki sekta ya uchumi wa baharini baada ya kukutana na wawekezaji na baadhi ya viongozi serikalini.

Bw Mung’aro alisema katika ziara yao, magavana walipata fursa ya kufanya mazungumzo na Waziri wa maswala ya kigeni wa Italia kuhusu vyeti vinavyotakiwa ili kusafirisha mazao ya Pwani.

“Tuna matumaini makubwa sana na ziara yetu baada ya kukutana na wawekezaji mbali mbali na hata serikali ya Italia. Tunalenga soko la bara Uropa ili kufungua nafasi za ajira na kupata soko la mazao yetu ya Pwani. Tunataka tununue mashua makubwa ambayo yatasaidia wavuvi wetu kuvua samaki wakubwa ambao tutaongeza thamani tukauze ulaya,” alisema Bw Mung’aro.

Magavana hao walisema wamepatia kipaumbele sekta ya uchumi baharini ili kufufua uchumi wa eneo hilo na kusaka nafasi za ajira.

Viongozi hao wanakabiliwa na changamoto ya ajira huku maelfu ya vijana wakiendelea kuwashinikiza kusaka mbinu za kukabiliana na swala hilo.

Bw Mung’aro alisema sekta hiyo ndio itakayopanua nafasi za ajira huku akiwarai kina wanawake kujitosa kwenye uvuvi na kilimo.

“Tunataka wawekezaji kutusaidia kununua mashua makubwa ambayo yanaweza kuingia maji makuu ili wavuvi wetu wavue samaki wengi ambao tutawaongezea thamani ili tupate soko la kimataifa,” alisema Bw Gideon.

Kwa sasa wavuvi wengi hutumia madau madogo ambayo hayawezi kwenda bahari kuu kuvua samaki.

Magavana hao Bw Mung’aro (Kilifi), Abdulswamad Nassir (Mombasa), Fatuma Achani (Kwale), Dhado Godhana (Tana River), Issa Timamy (Lamu), na Andrew Mwadime (Taita Taveta) kupitia muungano wao wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani, wameweka tofauti zao za kisiasa ili kusaka wawekezaji ughaibuni.

“Lazima tushirikiane ili tuweze kuvuna kutoka kwenye raslimali yetu ambayo ni Bahari Hindi. Tumetambua uvuvi kama njia bora ya kupata mapato zaidi na ajira kwa vijana wetu. Lakini lazima tuongeze thamani kwa mazao yetu ili tupate soko la kimataifa,” alisema Bw Mung’aro.

Gavana huyo ambaye ana uhusiano wa karibu na Waitaliano kupitia marafiki zake akiwemo bwenyenye mashuhuri Bw Flavio Briatore, alisema alitumia fursa hiyo kusaka wawekezaji.

Alipokuwa meya wa Malindi zaidi ya miaka 15 iliyopita, Bw Mung’aro aliunda uhusiano wa karibu na waitaliano.

Bw Gideon alisema magavana wa Pwani wameamua kushirikiana ili kusaka wawekezaji na kuimarisha sekta mbali mbali ikiwemo uchumi samawati na kilimo.

Alisema wanapania kuongeza thamani ya mazao yao.

“Tunataka kupigana na njaa na hata kuhakikisha usalama wa chakula. Tunashirikiana na nchi ya Italiano ambao wameapa kutuletea miundo misingi bora, kuvutia wawekezaji, kuimarisha kilimo na kubadilisha maisha ya Pwani,” alisema kwenye mkutano baada ya kukutana na Naibu Waziri wa Uchumi na Fedha wa Italiano Bw Maurizio Leo na afisa mkuu wa shirika la Africa Work for Africa program Bw Fabrizio Cardillo.