Makala

Mahangaiko ya wagonjwa Taita mgomo wa wahudumu wa afya ukianza

Na LUCY MKANYIKA September 7th, 2024 2 min read

FAMILIA za wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali za Kaunti ya Taita Taveta wamelazimika kutolewa hospitalini kutokana na mgomo wa wahudumu wa afya ulioanza Alhamisi, Septemba 5, 2024.

Mgomo huo umeathiri utoaji wa huduma za afya katika eneo hilo na kulazimisha wagonjwa na familia zao kutafuta njia mbadala za kupata matibabu.

Wagonjwa waliokuwa wakipokea matibabu muhimu katika hospitali za umma wamelazimika kuondoka, na kusababisha familia nyingi kuhamishia wapendwa wao katika hospitali za kibinafsi.

Katika hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi, ambayo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi, sasa imebakia mahame kutokana na mgomo huo.

Hali kama hiyo imeripotiwa katika hospitali za Wesu, Mwatate na Taveta.

Bi Mary Mwambeo, mkazi wa Voi, alisema kuwa alilazimika kumhamisha mume wake kutoka hospitali ya Moi kutokana na mgomo huo.

“Mume wangu alikuwa katika hali mbaya. Mgomo ulipoanza, hatukuwa na la kufanya ila kumhamishia hospitali ya kibinafsi hapa Voi. Gharama ni kubwa sana, lakini tutafanya nini?” alisema.

Mgomo huo umeathiri sio tu wagonjwa waliolazwa katika wodi, bali pia wanaotafuta matibabu mengine hasa wale wenye magonjwa sugu ambao wanategemea matibabu ya mara kwa mara.

Bw John Mwangi, ambaye mama yake ana ugonjwa wa Kisukari, alieleza kufadhaika kwake.

“Tunaenda Moi kila mwezi kwa kliniki za wagonjwa wa sukari. Alikuwa na kliniki wiki ijayo na hivyo atalazimika kwenda kwa hospitali ya kibinafsi ambapo gharama zake ni ghali,” alisema.

Hospitali ya Moi ni hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo na hutoa huduma muhimu kama vile CT scan, kuoshwa figo, upasuaji, maabara, huduma za uzazi, na vitengo vingine muhimu.

Huku mgomo huo unapoendelea, wakazi wa kaunti hiyo wanakabiliwa na janga kubwa la afya kwa kufungwa kwa vituo vingine vingi vya afya.

Wahudumu hao walitoa malalamishi yao ambayo wanataka serikali hiyo ya kaunti kuyashughulikia.

Wanalalamikia kucheleweshwa kwa mishahara, ukosefu wa bima ya afya, kutolipwa kwa makato yao ya bima na mikopo, ukosefu wa dawa na vifaa vingine za hospitali, miongoni mwa masuala mengine.

Mgomo huo umekuwa na athari kubwa kwa jamii, huku idadi ya watu walio hatarini kama vile wazee, watoto, na wale walio na magonjwa sugu wakiathirika zaidi.

Serikali ya kaunti imetaja ucheleweshaji wa fedha kutoka kwa serikali kuu kuwa kikwazo kikubwa katika kutatua matatizo yao.

Hata hivyo, vyama vya wahudumu hao vimetishia kutorudi kazini hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa.

“Serikali ya kaunti haiko makini kusuluhisha masuala ambayo tuliwawekea mezani,” alisema katibu wa wahudumu hao Bw Richard Nyambu.