Mahakama yakataa ushahidi zaidi katika kesi dhidi ya Sonko
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, amepata ushindi baada ya mahakama kuu kutupilia mbali ombi la wakili aliyemshtaki kumharibia sifa katika usimamizi wa mali ya zaidi ya Sh50 bilioni ya bwanyenye aliyeaga miaka 16 iliyopita.
Jaji Janet Mulwa alikataa ombi la wakili Lucy Nyamoita Momanyi la kutaka aruhusiwe kuwaita mashahidi wengine wawili katika kesi dhidi ya Sonko.
“Hii kesi imekuwa hapa kortini kwa miaka 11 sasa na hukusema unataka kuwaita mashahidi zaidi. Ombi hii limepitwa na wakati. Lengo lako kuu ni kuchelewesha kuamuliwa kwa kesi hii uliyoshtaki mwaka wa 2014,” Jaji Mulwa alisema.
Jaji huyo aliongeza kusema kwamba wakili Nyamoita alikuwa na wakati mwingi wa kutafakari jinsi atakavyoendeleza kesi hiyo na idadi ya mashahidi atakaowaita kuthibitisha kwamba aliharibiwa sifa na kukejeliwa na Sonko 2012 alipokuwa Seneta wa Nairobi.
Sonko kupitia wakili wake Martin Mbichire alipinga ombi la Nyamoita kuruhusiwa kuwaita mashahidi zaidi akisema “wakili hakuwasilisha orodha ya wateja aliowapoteza kufuatia madai katika vyombo vya habari kwamba alimpora mjane wa James Bellhouse.”
“Mlalamishi amekuwa wapi miaka 11. Ombi hili la kutaka aruhusiwe kuwasilisha mashahidi zaidi limepitwa na wakati na kamwe halifai kuruhusiwa,” alisema Bw Mbichire.
Mahakama iliombwa itupilie mbali ombi hilo na kumwagiza Nyamoita afunge kesi yake.
Mahakama ilikubaliana na Sonko kwamba lengo la wakili Nyamoita ni kuchelewesha kuamuliwa kwa kesi hii na kumwamuru akamilishe kutoa ushahidi wake.
Pia jaji alisema kesi hii ilishtakiwa kortini 2014 na imekuwa kortini kwa takriban miaka 11 sasa.
Jaji alitiupilia mbali ombi la Nyamoita na kumwagiza Sonko afike kortini Machi 16,2026 kujitetea dhidi ya madai kwamba alimkejeli wakili.
Katika ushahidi aliowasilisha kortini Sonko amesema kwamba baada ya kumkabili Nyamoita katika Mahakama kuu ya Mombasa, mjane wa Bellhouse , Bi Joy Nadzua aliweza kupata baadhi ya mali zilizokuwa zimefishwa ikiwa ni pamoja na mamilioni ya pesa kwenye mabenki na hisa katika makampuni zaidi ya nane.
Pia Sonko ameeleza mahakama kwamba baadhi ya mali nyingine zilizopatikana ni ploti mbili katika ufuoa wa bahari za ukubwa wa ekari 80.
Kila ekari moja iko na thamani ya Sh600milioni-sawa na Sh48bilioni.
Nyamoita anayehudumu jijini Mombasa amemshtaki Sonko kwa kumfedhehesha.
Nyamoita aliambia mahakama kuu ilibidi ajiondoe katika udhibiti wa mali ya mfanyabiashara tajiri wa kaunti ya Kwale marehemu James Simon Bellhouse baada ya kuvurugwa na mwanasiasa huyu mwenye tajriba ya juu.
Nyamoita aliambia Majhakama kuu Milimani Nairobi kwamba Bw Sonko alimkejeli na kumvuruga katika Mahakama kuu ya Mombasa alipodai alikuwa amefuja mali ya marehemu Bw Bellhouse.
Wakili huyo alimweleza jaji kwamba Bw Sonko alimtusi kwa kudai alikuwa mwizi na mnyakuzi wa mali yam jane.
Pia alidai Sonko alimkejeli kwa kudai alikuwa amemlaghai mjane wa Bellhouse, Bi Joy Nadzua mali na pesa.
Bi Momanyi aliyetoa ushahidi kortini alidai mbali na kukaripiwa mahakamani, gavana huyu wa zamani Nairobi alikuwa amemharibia sifa wakati wa mahojiano katika kituo kimoja cha televisheni.
Bi Momanyi aliambia mahakama kwamba mnamo Januari 10 2007 Bw Bellhouse alifika katika afisi yake ya mawakili na kuandika WOSIA ambapo alimteua (lucy nyamoita momanyi) na mkewe Joyce Nadzua kuwa wasimamizi na wathamini wa mali yake atakapoaga.
Bellhouse aliaga 2009 ndipo Bi Momanyi na Nadzua wakaanza usimamizi wa mali yake.
Pia walimzika eneo la Shimba Hills kwa misingi na itikadi za Kikristo ,kama alivyokuwa amewataka katika Wosia aliokuwa ameuandika.
Katika Wosia huo Bellhouse alikuwa amemtaka Bi Momanyi na Nadzua wamzike katika shamba lake lililoko Shimba Hills kaunti ya Kwale.
Wakili huyo alidai alipokabiliwa na Sonko mahakama kuu vyombo vya habari vilipeperusha mtafaruku huo na kusababisha wateja wake wakili huyo kumtoroka.

Aliambia mahakama alipata pigo kubwa na kusombwa na msongo wa mawazo.
Mbali na makabiliano hayo mahakama ya Mombasa, Bi Momanyi alishtakiwa kwa chama cha mawakili nchini LSK, ripoti za madai ya ufujaji wa mali ya Bellhouse kupelekwa kwa idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) na tume ya kuchunguza ufisadi (EACC).
Mlalamishi (Momanyi) huyo ameomba mahakama imwagize Sonko alimlipe fidia kwa kumharibia sifa na kusababisha wateja wake kumtoroka.
Lakini Bw Sonko amekanusha madai hayo ya wakili Lucy Nyamoita Momanyi na kusisitiza kwamba hakumharibia sifa kamwe.
Sonko aliambia mahakama Oktoba 23,2025 kwamba mjane wa Bellhouse, Joy Nadzua alimwendea mwaka wa 2012 alipokuwa Seneta wa Nairobi na kumsihi amsaidie kurudishiwa mali ya mumewe iliyokuwa inasimamiwa na Nyamoita.
Mjane huyo alimkabidhi Sonko WOSIA uliodaiwa uliandikwa na marehemu mumewe.
“Niliwapa mawakili wangu WOSIA huo kuukagua. Mawakili walinieleza kwa mujibu wa sheria Wosia huo haukuwa halali,” Sonko ameeleza mahakama kuu.
Sonko alisema mjane huyo alikuwa amemweleza kwamba ijtihada zake kupata ukweli wa mali ya mumewe mwendazake kutoka kwa wikili huyo zilikuwa zimegonga mwamba.
“Mjane alimweleza Nyamoita endapo hatamweleza bayana kuhusu mali ya mumewe itambidi asake msaada wa Mwanasiasa mwenye ushawishi,” Jaji Mulwa aliambiwa.
Sonko aliambia mahakama kwamba wakili huyo pia alimharibia sifa kwa kudai alikuwa mfungwa na kwamba alisababisha apoteze Sh16milioni.
Bw Sonko ameomba mahakama kuu ifutilie mbali kesi hiyo akisema kesi hiyo haina mashiko kisheria. Aliongeza kueleza korti,“sikumuharibia sifa wakili Lucy Nyamoita Momanyi na sifai kamwe kuadhibiwa.”
Kesi itaendelea Machi 16,2026.