• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
2018: Mwaka wa masaibu tele kwa Prof Swazuri

2018: Mwaka wa masaibu tele kwa Prof Swazuri

NA FAUSTINE NGILA

MWAKA huu umekuwa na changamoto si haba kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini (NLC) Prof Muhammad Swazuri, kuanzia Februari hadi Desemba.

Februari

Masaibu yake yalianza Februari 20 iliporipotiwa katika Kaunti ya Kwale kwamba watu kutoka Nairobi walivamia ranchi moja na kudai kuimiliki.

Kulingana na mshirikishi wa masuala ya ardhi katika ukanda wa Pwani, Bw Nagib Shamsan, tatizo la uskwota na mashamba Pwani linaendelea kwa kuwa serikali haiko tayari kulishughulikia.

“Katika ripoti ya Jopo la Njonjo tuligundua kwamba kuna familia 128,900 ambazo ni maskwota katika eneo la Pwani. Wenye mashamba wasiokuwepo wanamiliki ekari 77,753 za mshamba katika eneo la Pwani,” alisema.

“Hivi majuzi, Tume ya Ardhi nchini (NLC) kupitia kwa mwenyekiti wake Prof Muhhamad Swazuri ilitangaza kwamba itaanza kuchukua ardhi za mabwenyenye na kuwagawanyia wananchi.”

“Lakini lazima tufahamu kuwa Prof  Swazuri na wengine waliowahi kushughulikia suala la ardhi walisema hayo na bado hakuna kitu ambacho wametekeleza. Serikali haina nia ya kumaliza shida za mashamba katika Pwani,” akasema  afisa mkuu wa shirika la Kenya Land Alliance,  Bw Odenda Lumumba hapo Februari 20.

Machi

Na hapo Machi 14, NLC ilishindwa kuwashawishi wabunge iwapo Sh2.1 bilioni ilizolipa kama ridhaa kwa ardhi zilizotwaliwa na serikali kwa ujenzi wa miradi ya miundomsingi ziliwakilisha thamani halisi ya vipande husika vya ardhi.

Miradi hiyo ni kama vile ujenzi wa bandari ya Lamu, barabara za Outering (Nairobi) na Dongo Kundu (Mombasa).

Wakihojiwa na wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) kuhusu suala hilo, maafisa wa tume hiyo wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti Porof Mohammed Swazuri walikiri kwamba hawakuwasilisha stakabadhi za malipo kwa mhasibu mkuu wa fedha za serikali kwa wakati.

“Ni kweli kwamba tulichelewa kuwasilisha maelezo muhimu kama vile nambari za ploti, ekari za ardhi husika, ripoti ya utathmini wa ardhi na stakabadhi za benki kwa maafisa kutoka afisi ya mkaguzi wa hesabu kwa wakati uliowekwa.” Usemi huu uliwakera wabunge.

Juni

Katika mwezi huu mzee mmoja mwenye umri wa miaka 72 alishtakiwa Juni 13 kwa ulaghai wa Sh12 milioni, thamani ya shamba moja la mtaa wa Karen, Nairobi.

Bw Kuldip Singh Jandu alikanusha mashtaka mawili ya kumlaghai mfanyabiashara Shamir Dharamshi Radia.

Shtaka lilisema Bw Jandu alitumia barua aliyodai iliandikwa na kutiwa saini na Prof Swazuri mnamo Novemba 8, 2013.

Bw Jandu alikana kuwa alitumia barua hiyo kupokea kwa njia ya udanganyifu Sh12 milioni kutoka kwa Bw Radia akidai shamba la Karen lilikuwa lake na angelimuuzia.

Hata hivyo, jina la Prof Swazuri lilizidi kupakwa tope, hii ikiwa tu moja ya kesi nyingi ambazo anadaiwa kutia saini

Agosti

Huu ulikuwa mwezi wa masaibu tele kwa Prof Swazuri huku akikabiliana na mkono wa sheria na kupoteza kazi.

Mnamo Agosti 11, afisa huyo alikamatwa asubuhi dakika chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kusema ana kesi ya kujibu kufuatia sakata ya ulipaji ridhaa kwa ardhi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Bw Haji alisema Swazuri, naibu wake Abigael Mbagaya, Afisa Mkuu wa NLC Tom Chavangi na Mkuregenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini (KR)  Atanas Maina walifaa kukamatwa kutokana na sakata ya ulipaji wa Sh221 milioni, kama fidia kwa ardhi ambayo serikali ilitwaa kisheria kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Na hapo Agosti 16, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa NLC Bi Abigael Mbagaya Mukolwe aliteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti wa tume hiyo wakati ambapo mwenyekiti Prof Swazuri alikuwa anakabiliwa na kesi mahakamani.

Kwenye taarifa, NLC ilikana madai kuwa ilikuwa inakabiliwa na pengo la uongozi kufuatia kushtakiwa kwa mwenyekiti pamoja na maafisa wengine, ikisema Bi Mukolwe ametosha mboga kutekeleza majukumu ya mwenyekiti.

Mnamo Agosti 28, Mwakilishi Mwanamke wa zamani wa Kaunti ya Lamu, Bi Shakila Abdalla alitisha kumshtaki Prof Muhammed Swazuri na tume yote kwa jumla kufuatia kile alichodai kuwa ni kuwasaliti wakazi wa Lamu na kukandamiza haki yao ya kumiliki ardhi.

Bi Shakila alisema Swazuri alikuwa mstari wa mbele kutwaa ardhi za Lamu kiholela na kwa lazima kwa madai kwamba zilifaa kuendelezewa miradi ya kitaifa.

Bi Shakila alisema idadi ya maskwota kaunti ya Lamu imekuwa ikiongezeka kila kuchao hasa tangu tume hiyo ilipoanza kuhudumu hapa nchini.

“Tunaambiwa ardhi zimetwaliwa kufanikisha miradi ya serikali na maendeleo mengine. Kwa nini Swazuri ametusaliti namna hii? Hatutakubali na tuko tayari kutafuta haki yetu kisheria kama suala hilo halitazingatiwa na watu wetu kupewa haki yao ya kumiliki ardhi,” akasema Bi Shakila.

Desemba

Mwezi huu Prof Swazuri hakufurahia Krismasi kwani shirika moja la kutetea haki za umiliki wa aradhi lilitisha kuchochea umma likisema lazima akome kuvuruga ushahidi katikakesi inayomkabili mahakamani.

Hapo Desemba 24, shirika la Nation of Patriots likiongozwa na kiongozi wao Bw Abdulrahman Busera, lilimpa Swazuri makataa ya siku saba kukoma kuingilia utendakazi wa tume hiyo. Hii ilikuwa baada ya kompyuta yenye ushahidi kutoweka kutoka afisi za NLC.

“Iwapo Prof Swazuri hatakoma kuzima ushahidi dhidi yake, basi tutawachochea wananchi wazalendo kumkamata popote watampata na kumwasilisha kwa asasi husika,” akasema Bw Busera alipowahutubia wanahabari jijini Nairobi.

“Sisi kama wazalendo tunaunga mkono vita dhidi ya ufisadi. Lakini ulafi wa watu wachache wanaojitakia makuu unalemaza vita hivi. Hii ndio maana tunaitaka serikali kuhakikisha Prof Swazuri amefuata masharti yote ya dhamana,” akaongeza.

Aidha, waliwakosoa wafisadi ambao wamekuwa wakisema kabila lao linalengwa kwenye vita dhidi ya ufisadi kwa kuwa wanapopora mali, hawafanyi hivyo kuwafaidi watu wa kabila lao bali wao wenyewe.

“Tuna hakika kwamba Prof Swazuri aliingilia ushahidi katika kesi inayomkabili ili kupunguza uzito wa kesi hiyo. Tukiitwa kutoa ushahidi kuhusu suala hili tutautoa bila wasiwasi wala uoga,” akasema Bw Busera.

Walitoa wito kwa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) kuchunguza madai kuwa stakabadhi za ushahidi dhidi ya Prof Swazuri zilivurugwa, ndani ya NLC.

 

 

You can share this post!

AKILIMALI: Teknolojia mpya ya kukuza viazi inavyowapunguzia...

Mpango wa upangaji uzazi wazinduliwa Lamu

adminleo