2018: Uhamisho wa walimu ulizua utata baina ya KNUT na TSC
Na WANDERI KAMAU
MWAKA huu ulikuwa mgumu sana kwa walimu, hasa wanaofanya kazi katika ukanda wa Kaskazini Mashariki kutokana na msururu wa mashambulio kutoka kwa baadhi ya wakazi na kundi la Al Shabaab.
Mamia ya walimu walihama kutoka kaunti za Mandera, Wajir na Garissa— wakitaja maeneo hayo kuwa magumu kwao kufanyia kazi.
Mnamo Mei, walimu 224 kutoka shule za msingi na 42 kutoka shule za upili katika Kaunti ya Wajir walitangaza kuondoka humo baada ya wenzao wawili kuuawa na watu walioaminika kuwa wanamgambo wa Al Shabaab mnamo Februari.
Walimu hao waliuawa kwa kutokuwa wafuasi wa dini ya Kiislamu.
Kutokana na hayo, ilibidi Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kuingilia kati na kuwahamisha walimu 329 katika maeneo salama.
Wengine walilazimika kuondoka kwa njia zao wenyewe.
Kijumla, ilikadiriwa kwamba walimu 917 wa shule za msingi waliondoka katika eneo hilo.
Baada ya TSC kuonekana kutoshughulikia maslahi yao, zaidi ya walimu 120 walipiga kambi katika makao makuu ya Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) jijini Nairobi kwa zaidi ya miezi miwili kuishinikiza kuilazimisha TSC kuwahamishia maeneo salama ya kufanyia kazi pamoja na familia zao.
Ilibidi Katibu Mkuu wa KNUT, Wilson Sossion, kuingilia kati na kuishinikiza tume kuwahamishia walimu katika maeneo wanayohisi salama kufanyia kazi.
“Huu mfumo wa kuwalazimisha walimu kufanya kazi katika maeneo wanamokataliwa tumeupinga. Wao ni wafanyakazi ambao wana haki za kudai mazingira bora ya kufanyia kazi,” akasema Bw Sossion.
Katika mojawapo ya vikao, baadhi ya walimu walidondokwa na machozi wakati wakielezea masaibu ambayo walikuwa wakipitia mikononi mwa wasimamizi wa shule, wakazi na wanamgambo wa kigaidi katika maeneo hayo.
Malalamishi hayo yalizua majibizano makali kati ya KNUT na TSC, huku walimu wakitishia kufanya mgomo ikiwa tume haitasitisha mfumo huo wa uhamisho.
Katika kujitetea kwake, TSC ilisema kwamba mfumo huo unalenga kuleta “mshikamamo wa kitaifa” hivyo haingeusitisha hata kidogo.
Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Nancy Macharia alieleza kwamba kabla ya kumhamisha mwalimu yeyote, huwa wanazingatia taratibu zote za kisheria zinazohusiana mwongozo wao wa utendakazi.
Ni majibizano yalizozua hisia kiasi cha Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati.
Mnamo Agosti, Rais Kenyatta alisema kuwa TSC inapaswa kutathmini upya mfumo huo ili kuhakikisha kwamba hausambaratishi misingi ya familia za walimu.
Rais alisema kwamba alikuwa amepokea malalamishi kutoka kwamba uhamisho huo umesababisha baadhi ya famikiua kutengana.
“Tutatathmini upya mfumo huo ili kuhakikisha kwamba uhamisho wa walimu hautekelezwi ili kuonekana kama adhabu kwao ama kuvunja ndoa zao,” akasema Rais.
Alisifia sekta ya elimu, akisema kuwa inachangia pakubwa katika utimizaji wa Ajenda Nne kuu za Maendeleo za Serikali.
Na licha ya agizo la Rais, Bi Macharia alisema kuwa tume hiyo ndiyo yenye usemi wa mwisho kwani uhamisho ni mojawapo ya taratibu ambazo huwa inafanywa katika ulainishaji wa utendakazi kwa taaluma ya ualimu.
TSC ilianza kutekeleza mfumo huo mnamo 2017 ambapo zaidi ya walimu 1,065 wamehamishwa katika maeneo mbalimbali tangu kuanza kwake.
Licha ya agizo la rais, makabiliano mengine yanatarajiwa kati ya asasi hizo mbili kuanzia Januari 2, baada ya KNUT kupinga hatua ya TSC kuwahamisha zaidi ya walimu 3,094 majuzi.
Bw Sossion anashikilia kuwa kama kawaida, uhamisho huo ulifanywa bila kuwashirikisha ifaavyo.