Ada za e-Citizen zilivyoletea serikali ya Hasla Sh100 bilioni ndani ya mwaka mmoja
SERIKALI ilikusanya angalau Sh127.2 bilioni kupitia mtandao wa e -Citizen tangu Rais William Ruto alipoagiza huduma zote za serikali zilipiwe kupitia nambari moja ya malipo.
Waziri wa Fedha John Mbadi alisema jukwaa hilo linashughulikia maombi 120,000 ya huduma kila siku na liliweza kukusanya Sh26.4 bilioni katika mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 30, 2023.
Kiasi hicho, hata hivyo, kiliongezeka kwa kasi hadi Sh100.8 bilioni katika mwaka wa kifedha unaoishia Juni 30, 2024 huduma zaidi zilipowekwa kwenye jukwaa hilo ambalo kwa sasa lina huduma 16,000 za serikali.
“Tumefanikiwa kupunguza uvujaji kwenye mfumo. Kuwa na nambari moja ya malipo kumefanikiwa na mwonekano wa shughuli zetu umeimarika. Jukwaa limefaulu kukomesha uvujaji,” akasema Bw Mbadi alipofika mbele ya Seneti Jumatano.
Waziri huyo alisema kuwa malipo ya Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) hivi karibuni yatawekwa kwenye mfumo wa malipo wa kidijitali kama sehemu ya sera ya serikali ya kuwa na huduma zote kupitia jukwaa hilo.
Hii ni sehemu ya hatua ya Kenya Kwanza kufanya malipo yote ya serikali kuwa ya kidijitali ili kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza gharama ya ukusanyaji na kuimarisha utoaji wa huduma.
Bw Mbadi alikuwa akijibu swali la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliyetaka kujua ada inayotozwa na malipo mengine yote ambayo hayakisi kwenye jukwaa yanakoishia.
Seneta huyo alitaka kujua ni nini kimesababisha mfumo wa e-Citizen kushindwa kuchakata na kuakisi malipo yaliyolipwa kwa baadhi ya taasisi kama vile Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) pamoja na hatua zilizochukuliwa kurekebisha hali hiyo.