Makala

Adhabu kali kwa anayerusha roho na ‘Under 18’ aliyedanganya ni mtu mzima

Na BENSON MATHEKA October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NIMEULIZWA na wasomaji kadhaa iwapo mtu anaweza kuadhibiwa kwa kushiriki tendo la ndoa au kuoa mtu wa umri wa chini ya miaka 18 ambaye alimdanganya kuwa ni mtu mzima.

Mmoja wa wasomaji hao pia alitaka kujua jinsi anaweza kuepuka adhabu ikigunduliwa alifanya mapenzi na mtu wa umri wa chini ya miaka 18.

Kwanza kabisa, ningeshauri watu wakome kabisa kumezea mate watoto.

Kushiriki tendo la ndoa au kinachohusiana na ngono na mtu aliye na umri wa chini ya miaka 18 ni unajisi.

Hivi ndivyo sheria inavyosema na adhabu yake ni kali sana.

Mtu anaweza kufungwa jela miaka mitano kwa kuoa msichana au kuolewa na mvulana aliye na chini ya umri miaka 18.

Hapa, sheria haibagui ni nani anayekosa, iwe ni mwanamume au ni mwanamke.

Kwa kosa hili, unaweza kutozwa faini ya Sh1 milioni au adhabu zote mbili, yaani utozwe faini kisha ufungwe jela miaka mitano.

Hivyo basi, ni muhimu kuhakikisha kuwa umri wa mchumba yeyote ni zaidi ya miaka 18.

Sheria haiwasazi pia wanaosimamia harusi ambayo mmoja wa maharusi ana umri wa chini ya miaka 18.

Mtu kama huyo anaweza kufungwa jela miaka mitano kwa kuruhusu watu wasiofaa kuoana kufunga pingu za maisha.

Mtu huyo anaweza kutozwa faini ya Sh300,000 au apewe hukumu zote mbili, yaani kufungwa jela na kutozwa faini kwa kufungisha ndoa ya watu wanaotoka makundi yasiyofaa kuoana kama vile mtu kumuoa dada yake au mtu kuolewa na mtoto wake au watu walio na uhusiano wa damu kuoana.

Ili kuepuka adhabu kwa kosa hili, mshtakiwa hulazimika kuthibitishia mahakama kwamba hakufahamu na hakuwa na uwezo wa kufahamu uhusiano wa wanandoa jambo ambalo linaweza kuwa gumu kwake.

Ni muhimu kufahamu kuwa ni makosa kwa mtu kutoa habari za uongo wakati wa kuwasilisha ilani ya kufunga ndoa au ilani ya kupinga harusi.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, mtu anayewasilisha habari za uongo katika ilani ya ndoa au ya kupinga ndoa inayopangwa, huwa anavunja sheria na anaweza kufungwa jela miaka miwili au kutozwa faini isiyozidi Sh2 milioni au hukumu zote mbili.

Hapa ni kumaanisha kuwa mtu akidanganya kuwa ana umri wa miaka 18 anaweza kuadhibiwa kwa kutoa habari za uongo kuhusiana na ndoa.

Ili kuepuka adhabu hii, hakikisha kuwa habari zote kuhusu ndoa au kupinga ndoa ni za kweli. Ikiwa utaepuka adhabu kwa kutoa habari za uongo, utalazimika kuthibitishia mahakama kwamba ulikuwa na sababu za kuamini yale uliyowasilisha ni ya kweli.

Hata hivyo, inaweza kuwa kibarua kuthibitishia mahakama haya.