Makala

AFYA: Jinsi ya kubaini na kujilinda dhidi ya maradhi ya shinikizo la damu

February 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANDISHI WETU

Maradhi yasiyosambazwa (NCD) husababisha vifo milioni 16 kabla ya waathiriwa kutimu umri wa miaka 70, huku asilimia 82 ya vifo hivi vikiripotiwa katika nchi zilizo na viwango vya chini na wastani kimapato.

Ulimwenguni, maradhi ya moyo yanawakilisha vifo vingi vinavyosababishwa na maradhi yasiyosambazwa sawa na watu milioni 17.5, ukifuatiwa na kansa (milioni 8.2), maradhi ya mfumo wa kupumua (milioni 4) na kisukari (milioni 1.5). Miongoni mwa hivi vifo, shinikizo la damu husababisha vifo milioni 9.4 kila mwaka.

Kwa hivyo shinikizo la damu ni tishio kwa afya ya umma hasa ikizingatiwa kwamba kwa kawaida huwa haina ishara kuonyesha kwamba kuna tatizo.

Maradhi haya kwa kawaida hayaonyeshi ishara hasa katika awamu za mapema na watu wengi hawagunduliki kuugua.

Kulingana na ripoti ya saba ya kamati ya pamoja ya kitaifa kuhusu kuzuia, kutambua, utathmini na matibabu ya shinikizo la damu (JNC7), vitengo vya shinikizo la damu ni (shinikizo la damu kwenye ateri misuli ya moyo inaponywea (systolic) < 120 na shinikizo la damu msuli wa moyo ukiwa katikati ya mipigo ya moyo (diastolic) < 80.

Shinikizo la damu likiwa katika viwango visivyo vya kawaida basi kipimo chako kitakuwa systolic 120-139 au diastolic 80-89, awamu ya kwanza ya shinikizo la damu ni systolic 140-159 au diastolic 90-99 na awamu ya pili ya shinikizo la damu ni systolic>_ 160 au diastolic >_100.

Baadhi ya masuala yanayoongeza hatari ya kukumbwa na hali hii ni viwango vya juu vya cholesterol, uzani mzito, kutofanya mazoezi ya kutosha, uvutaji sigara na kunywa pombe zaidi, viwango vya juu vya glukosi kwenye damu, kisukari na uzee.

Kuna manufaa mengi ya kiafya na kiuchumi endapo tatizo hili litagundulika mapema ikiwa ni pamoja na tiba ya mapema na udhibiti wa shinikizo la damu.

Kutibu matatizo yanayotokana na shinikizo la damu huhusisha taratibu ghali kama vile upasuaji, cardiac bypass surgery, upasuaji wa carotid artery pamoja na dialisisi; taratibu ambazo hugharimu pesa nyingi.

Shinikizo la damu laweza kuzuiwa ambapo kufanya hivyo kunapunguza gharama za matibabu na ni salama kwa waathiriwa, ikilinganishwa na upasuaji kama vile bypass surgery na dialisisi, taratibu ambazo huenda zikahitajika iwapo maradhi haya yatagundulika mapema.

Njia nzuri za kujilinda kutokana na shinikizo la damu ni kufahamu hatari zinazoyasababisha na kufanya mabadiliko maishani.

Kwa hivyo ni muhimu kujihusisha na maisha yenye afya katika awamu zote za maisha. Kwa kiwango cha jamii kunapaswa kuwa na mipango ya uhamasishaji na uelimishaji kuhusiana na mradhi haya.

Uchunguzi wa mapema na kila mara kupitia vikao vya uhamasishaji, mipango ya afya shuleni na kazini, ni muhimu. Kupunguza kiwango cha chumvi kwenye chakula kutasaidia kuzuia na kudhibiti shinikizo la damu.

Kibinafsi, hatua zifuatazo ni muhimu katika jitihada za kuzuia shinikizo la damu: kuacha kuvuta sigara, kupunguza kula mafuta na badala yake kula vyakula kama vile njugu, mafuta ya mboga na samaki, kupunguza kula vyakula vilivyo na viwango vya juu vya cholesterol, kuongeza vyakula vyenye viwango vya juu vya nyuzi.

Hii husaidia kuondoa viwango vya cholesterol kwenye damu. Nyuzi zinapatikana kwenye shayiri, matunda, vyakula jamii ya maharagwe na nafaka ambazo hazijakobolewa.

Dumisha body mass index BMI (uzani wa mtu ikigawanyishwa na kimo cha mhusika kwa mita) kati ya 18.5 kg/m2 na 23 kg/m2.

BMI ni kipimo cha uzani wa mtu kuambatana na kimo chake. Kupunguza uzani husidia kupunguza kiwango cha cholesteraol mwilini.

Kufanya mazoezi kwa dakika 150 kila wiki pia ni muhimu.