Afya na Jamii

Huku Nairobi, kuna wakazi wanaenda haja chumbani na kurusha choo mtoni wakijificha

Na FRIDAH OKACHI October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VYOO katika mtaa wa Mukuru Kayaba jijini Nairobi viko katika hali mbaya huku sehemu ya wakazi ikikosa pa kuendea haja.

Mvua kubwa zilizoshuhudiwa mwezi wa Aprili na Mei 2024 zilisababisha mafuriko ya uharibifu kiasi cha kusomba vyoo.

Wakazi wanaoishi karibu na mito wamelazimika kuondoka ili kuishi umbali wa mita 30 kutoka kwenye mito.

Baada ya kukumbwa na hasara, wakazi sasa wanataabika baadhi wakitumia mifuko ya plastiki kuendea haja kubwa na kuitupa mtoni.

Watoto ambao wana uwezo wa kuenda msalani pia wanalazimika kutumia choo cha watoto kwa kimombo baby potty.

Bi Christine Maingi kutoka kijiji cha Kisii, ni miongoni mwa wale wanaotumia mifuko ya plastiki huku wanawe wawili wanaoenda shuleni wakitumia potty kutokana na hali kuwa mbaya zaidi.

Taifa Dijitali ilifahamishwa kuwa hali hiyo inazidi kuzoroteka kutokana na choo kimoja kutumika na nyumba kumi. Baadhi ya nyumba zikiwa na zaidi ya wanajamii watatu.

“Nalazimika kutumia beseni nyakati za usiku huku wanangu wakilazimika kutumia ‘potty’,” alisikitika Bi Maingi.

“Ndani ya chumba hiki, leso ndiyo inaficha siri zetu kutenganisha sehemu ya malazi na maeneo mengine chumbani. Kila asubuhi mimi humwaga uchafu katika mto Ngong.”

Bi Maingi anasema hali hiyo imesababisha kukosa siri na kuleta aibu ndani ya nyumba yake kwani anaishi na wavulana wake wawili waliobaleghe.

“Wakati mwingine ni vigumu hata kukaa usiku mzima na uchafu ndani ya nyumba ndogo,” anasema Maingi.

Bi Cecilia Wanyoike hakuwa na wazo kuwa ungekuwa mwanzo wa kukosa makazi na kuishi katika mazingira machafu baada ya kuhamishwa na mafuriko.

“Nakumbuka mwenye nyumba akiniharakisha niondoke ili kuokoa mabati, milango na madirisha ili mali yake isiibwe wakati wa ubomozi,” anasema Bi Wanyoike.

Alihamia nyumba nyingine, sehemu hiyo ikikosa choo baada ya kukosa msaada wa Sh10,000 ambazo zingemwezesha kutafuta makazi bora.

“Watu wengi hadi sasa wanaishi bila vyoo, wengine wamejenga vyoo kutumia magunia na vifaa vingine ili kutumiwa na watu 200-300. Tatizo ni kwamba unapata kuna foleni ndefu na ni chafu Zaidi.  Chooni, ukitazama sehemu ya juu, imegeuka na kuwa na rangi ya njano kwa sababu hakuna anayekubali kuvisafisha,” anasema Wanyoike.

Mhudumu wa Afya ya Jamii kutoka makazi ya Mukuru Kayaba, Bi Beatrice Omosa anasema ukosefu wa vyoo, umesababisha kuwapeleka wanawake wanane hospitalini kupata tiba kwa kupatwa na maradhi ya sehemu ya uzazi.

“Juhudi zangu kama mhudumu wa afya ni kuangalia hali ya wagonjwa nyumbani na mara nyingine wakazi wanaogopa kuzungumza nami kwa sababu bado wanahifadhi uchafu ndani ya nyumba zao wakichelewa kuutupa,” alieleza Omosa.

Kulingana naye, baadhi ya wakazi wanaogopa kufungua milango kutokana na uvundo wa uchafu.

Baadhi ya vyoo vinavyotumika Mukuru Kayaba. Picha|Fridah Okachi

Suluhu ya usafi katika mtaa wa Mukuru Kayaba

Kundi la Nyakwerigeria katika kijiji cha Kisii limejenga vyoo saba ambavyo, mkazi analazimika kulipa Sh 10.

Mwanachama wa Nyakwerigeria Bi Lucy Barasa alisema Sh 10 zinagharamia huduma ya kutoa sabuni na maji ya kunawa mikono baada ya kutumia vyoo, kuosha na kusalia safi.

Kwa watoto wakilazimka kulipia Sh 5 na Sh 30 kwa watu wenye familia.

“Tunaelewa kwamba kuna wale wasio na pesa, hatuwafukuzi wanapokuja, tunawahudumia bure. Hii ndiyo suluhisho pekee la tatizo la vyoo katika eneo hili,” alisema Bi Barasa.

Naibu Kamishna Kaunti Ndogo ya South B, Bw Ndambuki Kimeu alisema kuwa kama serikali, wana mipango ya kusaidia watu kupata mazingira safi na salama.

Alihimiza wamiliki wa nyumba kutumia vyoo vya Fresh Life ambavyo havihitaji mifereji.

“Tunavyo vichache kando ya ardhi ya ukingo wa mto, na mpango wa mwisho ni utekelezaji wa sheria, mmiliki yeyote wa nyumba anayeelekeza uchafu mtoni atakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Bw Kimeu.