Afya na Jamii

Jinsi kansa ya ovari inavyolemea wanawake, mifumo ya afya na serikali kiuchumi

Na PAULINE ONGAJI September 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KENYA ni mojawapo ya mataifa ambayo yameathirika pakubwa kiuchumi na katika mfumo wa afya, kutokana na maradhi ya kansa ya ovari.

Haya ni kulingana na utafiti uliofadhiliwa na Muungano kuhusu maradhi kansa ya ovari (World Ovarian Cancer Coalition), shirika lisilo la kiserikali linaloshirikiana na zaidi ya mashirika 200 ya wagonjwa wa kansa ya ovari, kutoka mataifa 37.

Kwa mujibu wa utafiti huu, maradhi haya hayaathiri tu wagonjwa, bali yana athari kubwa katika uchumi na mifumo ya afya ya mataifa husika, huku hasara hii ikitokana na gharama ya matibabu, vile vile kufifia kwa utendakazi kwa walioathirika.

Utafiti huu ulichanganua athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na kansa ya ovari katika mataifa 11, yanayowakilisha maeneo tofauti na viwango tofauti vya kiuchumi (ikiwa ni pamoja na Kenya, Malawi, Nigeria, Australia, Canada, Colombia, India, Kazakhstan, Malaysia, Uingereza, na Amerika).

Utafiti huu unakadiria kwamba katika mwaka wa 2023, mataifa haya yalishuhudia hasara ya kufikia Dola 69.9 bilioni za Amerika kutokana na maradhi haya, huku hasara kuu ikiwa katika mifumo ya afya, ambapo gharama ya matibabu na kufifia kwa uwezo wa kufanya kazi miongoni mwa waathiriwa, kulikuwa na mzigo kwa uchumi.

Kulingana na utafiti huo, wanawake wanaougua kansa ya ovari hupoteza takriban siku milioni 2.5 za kazi kwa sababu ya ugonjwa huu, na zaidi ya wanawake 9,400, wanaoishi na maradhi haya au wamepona, wanakadiriwa kutoweka kwenye orodha ya wafanyakazi.

Hasara hii haihusishi tu wagonjwa wanaougua kwani kila mhudumu alitumia takriban siku 33 kutoa huduma kwa wagonjwa, na hivyo kuathiri maisha yao hasa ya kiuchumi.

Kulingana na Bw Mikis Euripides, anayehusika na mawasiliano kuhusiana na utafiti huu, mataifa haya 11 yalichaguliwa kuwakilisha viwango tofauti vya kiuchumi kulingana na Benki ya Dunia, vile vile pia kuhakikisha uwakilishi wa kimaeneo katika mabara yote.

“Shughuli ya kuchagua mataifa haya ziliangazia maeneo ambayo muungano huu umeunda mahusiano thabiti na pia kufanya tafiti za awali za wagonjwa,” alieleza Bw Euripides.

Kansa ya ovari ni mojawapo ya saratani hatari zaidi ulimwenguni. Duniani, zaidi ya wanawake 900,000 wamegundulika kuugua kansa ya ovari katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku wanawake saba kati ya kumi, wakigundulika maradhi haya yakiwa katika awamu sugu.

Nchini Kenya, kansa ya ovari ni ya pili miongoni mwa aina ya saratani za uzazi zilizokithiri zaidi, huku ikiwakilisha asilimia 4 ya visa vyote vya kansa.

Kutoka mwaka wa 2022 kufikia 2050, inakadiriwa kwamba maradhi haya yatasababisha vifo vya watu takriban milioni nane.

Aidha, utabiri wa mwaka wa 2022 wa mtandao wa kuchapisha takwimu na utafiti kuhusu kansa wa Globocan, unaonyesha kwamba, kufikia mwaka wa 2050 idadiya wanawake wanaogundulika kuugua kansa ya ovari itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 55 na kufikia 503,448, huku vifo vya kila mwaka vinavyosababishwa na maradhi haya vikiongezeka kwa takriban asilimia 70 na kufikia 350,956.

Mataifa ya uwezo duni na wa kadri kiuchumi ndio yatakayoathirika pakubwa kwani asilimia 70 ya wanaogundulika kuwa na maradhi haya, wanatoka katika mataifa haya.