Afya na JamiiPambo

Kufuatanisha watoto kwa karibu kutafanya uzeeke upesi, utafiti

Na MARY WANGARI  November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UJAUZITO NA UZAZI 

KUZAA watoto wakiwa wamefuatana kwa karibu bila muda wa kutosha kabla ya kushika mimba huenda kusababisha kuzeeka haraka, utafiti mpya umefichua. 

Kulingana na wataalam, kupachikwa mimba zikifuatana kwa karibu huenda kukazuia mwili kuwa na muda wa kutosha kupata afueni hivyo kusababisha mabadiliko yanayohusiana na kuzeeka kibiolojia kuongezeka. 

Utafiti huo ulitathmini mabadiliko kibayolojia yanayotokea mwanamke akiwa mjamzito kwa lengo la kuboresha afya ya ujauzito ulifichua uhusiano uliopo kati ya mimba na kuzeeka. 

Muda wa kupata afueni baada ya kujifungua na kubeba mimba nyingine huenda mwishowe ukaathiri afya ya mama ya muda mrefu, wataalam wanasema. 

Kutungwa mimba zinazofuatana kwa karibu kunaweza kuzuia kupona kikamilifu hivyo kuruhusu baadhi ya mabadiliko kuongezeka katika mimba zitakazofuata, wanafafanua. 

‘Utafiti wetu wa awali umebaini kuwa umri kibiolojia huongezeka kwa muda wakati wa ujauzito, na kufikia kilele katika kipindi cha tatu au wakati wa kujifungua,” wanafafanua wataalam kutoka Harvard Medical School. 

“Tukikubali wazo kuwa mabadiliko haya ya muda mfupi katika umri kibiolojia hutokea, swali ni jinsi tunaweza kuhusisha mabadiliko hayo kwa mkondo wa jumla wa kuzeeka maishani.” 

Japo kuna uwezekano kwamba huenda mkondo wa kuzeeka kwa jumla ukabadilika, wataalam wanafafanua kuwa hii sio sawa na uharibifu kibiolojia. 

“Tunafahamu kuwa sehemu fulani au kubeba mimba hadi miezi tisa ikamilike, kuna manufaa kwa maisha ya mtu binafsi.” 

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa linapendekeza kusubiri kwa muda usiopungua miezi 24 baada ya kujifungua salama kabla ya kutungwa mimba nyingine, kama namna ya kupunguza athari za afya kwa mama na mtoto. 

“Kuna mshawasha mkubwa kuhusu kutumia nyenzo za kutathmini umri kibiolojia kuelekeza umri wa mtu binafsi kwa kiwango cha kuzuia na kinachowiana na mhusika. Kuchunguza mabadiliko wakati wa ujauzito ni njia mojawapo ya kupata uelewa wa kimsingi kuhusu kuzeeka kwa upana.” 

Ili kutoa mapendekezo mahsusi kuhusiana na kuzeeka kibiolojia badala ya matokeo ya ujauzito, wataalam wanasema utafiti zaidi utahitajika kupima umri wa kibiolojia kwa mimba kadhaa na kisha kufuatilia kina mama husika kwa miongo kadhaa baadaye.