Afya na Jamii

Wafugaji Narok wateta uhamaji wa nyumbu husambazia ng’ombe ugonjwa hatari

Na KNA September 25th, 2024 2 min read

UHAMAJI wa nyumbu (wildbeast) ni tukio la ajabu ambalo huvutia watalii kutoka maeneo mengi duniani kuzuru Mbuga ya Wanyama ya Maasai Mara ili kuushuhudia ana kwa ana.

Hujiri kila mwaka ambapo mamilioni ya nyumbu huhamia Kenya kwa kuvuka Mto Mara kutoka Mbuga ya Wanyama ya Serengeti – Tanzania.

Msimu huu huanza mwezi Julai na kukamilika mwisho wa mwaka nyumbu wakirejea walikotoka.

Ni furaha kwa mamilioni ya watalii wanaovutiwa na tukio hili. Pia, ni furaha kwa mataifa haya yanayovuna mabilioni ya pesa. Lakini wafugaji na wakulima hawana furaha.

Wakulima wanateta kuwa ugonjwa unaosababishwa na virusi hubaki katika mazingira ambayo nyumbu hawa huzalia.

Kulingana nao, mifugo wao hula nyasi hapo na kuwa wagonjwa na wanyonge.

Mfugaji wa eneo la Emati, Kaunti Ndogo ya Trans Mara, Abraham Tobiko anasema kuwa sio nyumbu wote hurejea upande wa Tanzania kuzaa.

“Baadhi ya nyumbu hubaki Kenya kuzaa. Iwapo ng’ombe atakula nyasi za eneo ambapo nyumbu amezalia, hupata maradhi hatari ya kusababisha kifo,” alisema.

Bw Tobiko alisikitika kuwa ng’ombe wake alifariki akiamini alikula nyasi iliyoathiriwa na virusi.

“Tunapopata nyumbu wenye mimba karibu na makazi yetu, sisi huwafukuza ili wasizae karibu na maeneo yetu ya malisho,” aliendelea.

Ugonjwa wa virusi

Daktari wa mifugo eneo la Narok Magharibi Matthew Nchoko alithibitisha ugonjwa huo unaosababishwa na virusi akiutambua kuwa Malignant Catarrhal Fever (MCF) ambao huua mifugo.

Ng’ombe aliyeambukizwa huwa na mafadhaiko, huendesha, hukosa hamu ya kula, huwa na joto kali na kutiririsha makamasi akiwa katika hatari ya kufa.

Kwa mujibu wa Dkt Nchoko, asilimia kati ya 3 – 12 ya ng’ombe waliolishwa katika eneo ambapo nyumbu amezalia hufa kutokana na ugonjwa huo.

Uangalifu

Anawashauri wafugaji kuwa waangalifu wasiwalishe mifugo wao katika maeneo hatari akieleza kuwa ugonja huo hauna tiba.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Wanyamapori nchini (KWS) anayesimamia eneo la Narok Ibrahim Osman alisema nyumbu hulishwa katika sehemu iliyolindwa.

Kwa hivyo ameshauri wafugaji kuepuka kuwalisha ng’ombe wao katika maeneo ya mbuga ovyo ovyo.

“Hapo awali, nyumbu walikuwa wanazurura maeneo ya mbali, lakini kwa sababu ya kuwepo kwa makazi ya watu, wanalindwa ndani ya mbuga, ambapo ni makazi yao halisi,” alisema.

Osman alisema jamii ya wafugaji imeishi na wanyama wa msituni kwa miaka na hawajawahi kulalamikia ugonjwa huo.

“Nimesikia kuhusu ugonjwa huu lakini sina uhakika kama umethibitishwa kisayansi. Hata hivyo, ninawashauri wakulima wakae mbali na maeneo yanayolindwa, ambapo nyumbu hupatikana na kuzalia,” alisema.

Kwa nini nyumbu wanahama?

Kulingana na wataalamu uhamaji huu huchochewa na haja ya wanyama hawa kuzaa. Wao huingia Kenya kujamiana na kurejea Tanzania kuzaa.

Mwaka huu, angalau nyumbu milioni tatu wamevuka mpaka kutoka Serengeti hadi Kenya, ni idadi kubwa zaidi ya miaka iliyopita.

Takwimu hizi zimetolewa na Gavana wa Narok Patrick Ntutu ambaye anakiri sekta ya utalii eneo la Mara ni chanzo kikubwa cha mapato kwa Kaunti ya Narok.

Bw Ntutu anafichua kuwa utalii eneo la Mara huzalishia gatuzi hilo Sh3.5 bilioni kila mwaka.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan