Wanaume wanaolia na kuonyesha hisia zao ndio wapenzi bomba – Wataalam
WATAALAMU wa masuala ya mapenzi wamebaini kuwa wanaume wenye hisia kali kiasi cha kudondokwa na machozi kwa sababu ya wapenzi wao, huishia kuwa na uhusiano dhabiti wa kimapenzi.
Hii ni kinyume na dhana ya kipindi kirefu kuwa wanaume wenye misuli na kifua kilichotanuka ndio huwaniwa na wanawake kutokana na maumbile yao ya kupendeza.
“Sasa mambo yamebadilika, imebainika kuwa wanaume wanaodondokwa na machozi hata kwa mambo madogo wana utu, wenye huruma na hunogesha mapenzi,” anasema Marina Lazaris, Mtaalamu wa Masuala ya Mapenzi ambaye pia ni mchapishaji wa jarida la ‘Wanaume Huhitaji Mapenzi Pia’ linalochapishwa Amerika.
“Kutofautisha kati ya hisia ya kumwonea mtu imani, huruma na mwenendo wa zamani ambapo maumbile ndio huzingatiwa kama kigezo cha kupenda, ni jambo ambalo limeanza kuwachanganya wanaume,” anasema mtaalamu mwengine Adam Cohen Aslatei wa Shirika la Tawkify, Amerika.
Mtaalamu huyo ametoa ufafanuzi kuwa kumpata mwanaume ambaye hisia zake ni thamani kwake, kutawasaidia wanawake kuwapata wapenzi wa kudumu.
Mara nyingi wanawake wamelalamikia hatua ya baadhi ya wanaume kuwahadaa kwa kuanzisha uhusiano nao kimapenzi kisha kuwahepa.
Hii ni kwa sababu wanaume hao hawathamini hisia zao na hawaingii katika uhusiano huo na roho yote.
Kizazi cha sasa cha Gen Z kinaonekana kubadili tamaduni ya wanaume wazuri kuonekana kuwa wale waliojaa misuli na kutanuka kifua maarufu kama ‘six pack’.
Sasa wanawake wanawathamini wanaume ambao wanaweza kudondokwa na machozi kwa sababu yao, wanawathamini sana na hutetea haki zao kwa kukemea dhuluma wanazopitia katika jamii.
“Saa hii mambo si kujaza misuli na kutanuka kifua au kuwa mwanaume mwenye msimamo mgumu. Sasa ni uaminifu, mwanaume mlinzi, mwenye heshima na yule ambaye hisia zake zinaonyesha wazi mapenzi kwa mwanamke,” anaongeza Bi Lazaris.
Mtaalamu huyo anasema mabadiliko hayo yameanza kushuhudiwa kote ulimwenguni kwa sababu wanaume wengi sasa hawafichi hisia zao kwa hofu ya kuchekwa jinsi ilivyokuwa zamani.