Akili Mali

Anaongeza thamani matunda ya Zabibubata (Gooseberries)

Na PETER CHANGTOEK December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIOLA Maina alihudumu katika kampuni ya NMG kuanzia 2003 hadi 2017, kisha akajiuzulu ili kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani matunda ya zabibubata (gooseberries), ambapo aliasisi kampuni inayojulikana kama Gooseberry Delight Limited, linaloendesha shughuli zake katika eneo la Ilula, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alianza kwa kuyanunua matunda hayo kwa Sh30 na kuuza kwa Sh40 kutoka kwa mkulima mmoja.

Baadaye, wakulima wakaanza kuyazalisha matunda hayo kwa wingi, jambo lililomshurutisha kuwaza na kuwazua kuhusu uongezaji thamani, ili kuzuia kuharibika kwa matunda.

Alikuwa akitangaza biashara yake kupitia kwa mitandao ya jamii, na wakati mmoja akapata oda ya mikebe 500 ya matunda hayo kutoka kwa dukakuu moja jijini Nairobi na biashara ikaanza kuvuma.

Hata hivyo, ugonjwa wa Covid-19 ulipoenea nchini, biashara yake ikaathirika, japo ilianza kuimarika Septemba 2020.

“Nilipigiwa simu na mtu aliyekuwa akitaka kuuza ughaibuni. Sikuwa na kiasi alichokuwa akitaka, lakini wiki moja kabla ya wakati huo, nilikuwa nimepigiwa simu na mkulima mmoja wa kike kutoka Kitale, aliyekuwa na ekari 20. Nilienda Kitale na tukazungumza na hakuwa akijali kuhusu bei; tuliafikiana na nikapakia kwa gari na kuchukua hadi Nairobi,” asimulia, akiongeza kuwa, aliuza kilo moja kwa Sh160 na alipata fedha nyingi mno.

Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na Gooseberry Delight Limited. PICHA/PETER CHANGTOEK

Baadaye, alipata oda ya kilo 400 kutoka kwa mtaalamu mmoja wa lishe katika kampuni moja ya kutengeneza chakula jijini Nairobi.

Hata hivyo, alipopigiwa simu tena, hakuwa na matunda hayo. Baadaye, wakulima wakaanza kuzalisha kwa wingi, naye akaamua kupata mafunzo ya wiki moja kwa ada ya Sh10,000 katika taasisi ya Kirdi, ambapo alifunzwa jinsi ya kutengeneza jamu na juisi.

Kwa sasa, ana wafanyikazi 15; vibarua wanne na kumi na mmoja wa kudumu. Anaongeza kwamba, amekuwa akishirikiana mno na asasi mbalimbali, kama vile Kalro, Kirdi na Kaunti ya Uasin Gishu.

Anafichua kwamba, kwa wakati huu, hununua zabibubata kwa Sh50 kwa kilo, na kuyatumia matunda hayo kutengeneza sharubati, jamu na bidhaa nyingine.

Anasema kwamba ana wakulima wengi ambao wanaomwuzia zabibubata.

Kwa mujibu wa Viola ni kwamba, wakulima wanaotegemea mvua kuikuza mizabibubata, wanaweza kuchuma kilo 100 kila wiki, ilhali wale wanaonyunyizia maji wanaweza kuchuma hadi kilo 250 kwa wiki.

Baada ya kuyanunua matunda hayo, wao huchambua na kukausha kabla hayajachakatwa. Changamoto moja wanayopitia ni kupata vifaa vya kukaushia matunda.

“Hiyo ndiyo changamoto; tunahitaji kikausho,”

asema.

Wao huuza bidhaa zao za aina mbalimbali kwa bei kuanzia Sh130-Sh270. Anaongeza kwamba, tayari wamepeleka sampuli ya sharubati kwa shirika la Kebs, na wanasubiri idhini.

Baadhi ya wafanyakazi wa Gooseberry Delight Limited, wakionyesha baadhi ya bidhaa zao. PICHA/PETER CHANGTOEK

Hata hivyo, bidhaa zao nyingine zimeidhinishwa na Kebs.

Kampuni ya Gooseberry Delight Limited hununua aina mbili za matunda ya zabibubata; Colombian na Brazilian. “Tunashirikiana na Kalro. Walinipa mbegu na nikawaomba wanipe idhini ili nipande mbegu na niuze miche,” adokeza.

Viola anafichua kwamba, huuza miche ya mmea huo kwa Sh8 kila mmoja. Anaongeza kwamba, katika shamba ekari moja, miche inayofaa kupandwa ni 2,500.

Siku chache zilizopita, walipata fursa ya kutangaza bidhaa zao katika maonesho ya kililimo na biashara (ATF) katika Chuo Kikuu cha Eldoret. Aidha, wamepata fursa ya kuonesha bidhaa zao mjini Mwanza, Tanzania na nchini Uganda.

Anasema kuwa, ametumia takribani Sh3 milioni, na kuna wakurugenzi wengine wawili waliojiunga na kampuni hiyo mapema mwaka huu, ambao pia wamewekeza takribani Sh2 milioni kila mmoja.

Wao huziuza bidhaa zao katika madukakuu kadhaa nchini. Anaongeza kuwa, pesa nyingi kati ya hizo, zimetumika kufanya utafiti na kununua vifaa.