Akili Mali

Jinsi kundi la Joyful Birds linavyofaidi wanachama kwa ufugaji kuku

Na SAMMY WAWERU December 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA kitongoji cha Soweto, Kayole, Kaunti ya Nairobi, kundi moja la wafugaji kuku lina hadithi ya kuvutia jinsi lilivyoanzishwa.

Joyful Birds Self-Help Group, kundi la wanachama 21, liliasisiwa miaka kumi iliyopita kupitia wanachama wanaokiri waliunganishwa na jukwaa la kuchapa gumzo.

Soweto, ni mojawapo ya vitongoji duni Nairobi na wanachama hao ni wenyeji ambao wengi wao hawakuwa na ajira.

Kupitisha muda, walikuwa wakishiriki mazungumzo yaliyosheheni masengenyo.

“Tulianzisha Joyful Birds 2012 tukiwa wanachama wanane, ambao ni wakazi wa Soweto. Wengi wana familia ila hawana kazi. Walikuwa wakipoteza muda kwa kushiriki gumzo la fitina, ila jambo moja lilikuwa wazi; baada ya siku majukumu na bili zilikuwa zikiwasubiri,” anasema Timothy Malasi,

Kulingana Malasi, ni wanachama watatu pekee walikuwa na ajira, na kila walipotangamana walikuwa wakihurumia wenzao.

Baada ya muda, waliamua kutumia jukwaa la masengenyo kufanya jambo la busara.

Licha ya changamoto zilizowazingira, walikubaliana kuchanga Sh25 kila wiki – kila mhusika.

Jumapili, baada ya ibada ya kanisa Malasi anasema walikuwa wakikutana.

Walichanga kwa muda wa miezi mitatu mfululizo wakiweka hela hizo kama akiba.

“Kila aliyeshiriki mkutano na kuchanga alionekana mtu anayejua anachofanya,” Malasi anakumbuka.

Hatimaye, walitinga Sh5, 000 japo kuamua jambo ambalo wangefanya na pesa hizo ilikuwa kizungumkuti.

“Kumbuka, ni hela za watu waliopambana kukithi familia zao mahitaji muhimu ya kimsingi. Majaribu yalikuwa mengi,” anasema.

Maamuzi yaliafikiwa kupitia kisa cha mmoja wa wanachama aliyekuwa na hafla ya kuombea mwanawe na kuku ilikuwa chaguo la kupikia walioalikwa.

“Wazazi wake kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya na pasta walikuwa wageni mashuhuri, na mila na itikadi za anakotoka nyama za kuku ndizo zinathaminiwa,” Malasi anaelezea.

Mbele na nyuma, mwanachama huyo, Malasi anadokeza kwamba alikuwa na Sh3, 000 na alipozunguka masoko ya Kayole kuku mmoja alikuwa akiuziwa Sh2, 000, hii ikiwa na maana kuwa alikuwa na punguo la Sh1, 000.

Anasimulia kwamba alilazimika kuongeza hela hizo ili anogeshe hafla ya kuombea mwanawe.

“Mahangaiko aliyopitia yalitufungua macho tukaamua kuanzisha mradi wa kuku,” Malasi anadokeza.
Pesa walizoweka akiba, zikawa mtaji ambapo walianza na vifaranga 20, japo watano pekee ndio walifanikiwa kukua hadi wakakomaa.

Malasi anasema walikodi sehemu karibu na Mto Soweto, wakajenga vizimba.
Miaka 12 baadaye, Joyful Birds Self-Help Group inajivunia kuwa biashara iliyosajiliwa na yenye mashiko; inauza bidhaa za kuku na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia (JKUAT) na kile cha Kenyatta (KU), ni kati ya taasisi ambazo wanafunzi wake wanaosomea kozi za kilimo na ufugaji wamenolewa makali na kundi hilo

Wakati wa mahojiano, tulipata likiwa na kuku wapatao 650 idadi hiyo ikiwa ni punguo kutoka 1, 500 baada ya majengo yao kubomolewa Aprili 2024 kufuatia bomoabomoa iliyotekelezwa na serikali kuondoa waliojenga karibu na mito Nairobi.

Ubomoaji huo, uliwasababishia hasara ya mayai 500 ambayo yalikuwa kwenye mashine ya kuotesha na kuangua vifaranga yaliyoharibika.

“Shabaha yetu ilikuwa kufikisha kuku 2, 000. Ubomoaji haukutupa nafasi ya kupanuka,” Malasi anasikitika.

Joyful Birds imewekeza kwenye mitambo ya kuotesha mayai ya idadi jumla ya 1,056 na nyingine 300.
Kwa sasa, wanahudumu kwenye jengo la ghorofa mbili walilokodi ili kufufua biashara yao.

“Tukipata mdhamini atupige jeki, tutaangazia upungufu wa bidhaa za kuku jambo litakalofungua nafasi za ajira hasa kwa vijana,” anasema Mzee Patrick Atetu, mwanachama na mshauri wa mradi huo.

Biashara ya kundi hilo ni kuzua mayai, vifaranga na kuku waliokomaa.

Jitihada zao zimetambuliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na pia Maonyesho ya Kilimo Kenya (ASK) 2023 ambapo Joyful Birds iliorodheshwa miongoni mwa biashara tatu bora wakati wa maonyesho ya ASK Nairobi.