Kilimo bila Udongo: Ladona alivyopona baada ya kulea mboga za thamani kubwa
ALIANZA kukuza nyanya katika vivungulio (greenhouses) miaka minane iliyopita, lakini ushindani wa wakuzaji mboga kwa njia ya kawaida ulimpiga teke hadi nje ya soko.
Hapo ndipo aliamua kukumbatia njia maalum ya teknolojia ya kilimo bila udongo (hydroponics) na utumizi wa vivungulio ili kukuza mboga za thamani ya juu zenye soko maalum.
Bi Leah Ladona, 24, sasa amepona kwa kulea mimea kama vile nyanya aina ya cherry tomatoes, matango (cucumber) na pilipili mbalimbali kama vile pilipili hoho ya rangi kuvutia masoko ya hadhi.
“Hatua yangu ya kuzamia mboga za thamani kubwa imetokana na uchunguzi wa soko la bidhaa hizi katika maeneo ya mijini,” anasema Bi Ladona. “Teknolojia ya hydroponics inaniruhusu kuzalisha mazao bora ambayo yanahitajika sana na wateja wetu.”
Ni mwanzilishi wa Agroponics Enterprise, kampuni inayotatua matatizo ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia.
“Tunajivunia kwa kuzalisha mboga za kipekee na kutoa mafunzo ya kilimo, huduma bora za agronomia – ujuzi wa kilimo, na kuunganisha wakulima na masoko nchini,” aliambia Jarida la Akilimali.
Bi Ladona, ambaye ana shamba lake Kenyatta Road, eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu, anakuza mazao ambayo huchukua muda wa kati ya miezi mitatu hadi sita kukomaa.
“Ninapenda mimea hii kwa sababu zikianza kuchanua, matunda huota haraka na kupisha kipindi cha mavuno,” alisema. “Uzuri wa mboga hizi ni kwamba, pindi unapovuna mara ya kwanza, matunda hukua na kukomaa haraka tena.”
Bi Ladona, ambaye anadhihirisha kuwa na shauku ya muda mrefu ya kilimo, alianzisha Agroponics Enterprise mwaka 2016 akiwa mwanafunzi chuoni Kenyatta.
Kulingana naye, kujitolea kwake kustawisha kilimo bila udongo na matumizi ya mifumo ya umwagiliaji wa matone ndani ya vivungulio kumekweza ufanisi wa mbinu changamano katika sekta ya kilimo nchini.
“Tunauza mazao yetu hasa katika maduka makuu na pia shambani. Bidhaa zetu zina chapa inayotambulika na zimepata umaarufu mkubwa,” anasema Ladona. “Hatuuzi sana kwa mama mboga wa kawaida.”
Mtaalamu huyu wa kilimo anasisitiza umuhimu wa kudhibiti joto ndani ya vivungulio ili kuhakikisha mazao yanastawi vizuri.
“Kilimo cha mazingira bila udongo kinahitaji udhibiti sahihi wa hali ya joto, unyevu na mwanga,” anaeleza. “Joto huharakisha ukuaji na kukomaa kwa mazao.”
Kwa sababu vijana wengi wametamani kilimo hiki huku mitaala ya chuo ikitoa mafunzo ya teknolojia, wanafunzi wengi humiminika humu kwa masomo ya nyanjani.
Aghalabu Bi Ladona huwatumia wanafunzi hawa kuwa wafanyakazi wa shambani wanapoendelea kupokea mafunzo. Mintarafu hii, amepunguza gharama ya oparesheni.
Agroponics Enterprise inaamini kwamba kupitia jitihada zao za kilimo cha hydroponics, wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika mitindo ya kilimo nchini – ikisaidia wakulima kupata mapato bora na kuboresha maisha ya jamii.