AKILIMALI: Atia fora katika kilimo cha nyanya Vihiga
Na SAMMY WAWERU
KATIKA kijiji cha Kedeta, Kisienya, Kaunti ya Vihiga, wakazi wengi wamekumbatia kilimo cha majanichai.
Licha ya taswira hiyo, ukiingia katika boma la Bw Hesbon Asava, unaliona shamba kubwa la matunda aina ya maparachichi, maembe na ndizi.
Pembezoni mwa ndizi, ana kivungulio. Ndani yake kunakuzwa nyanya, spinachi, kabichi na mboga asilia aina ya mnavu.
Asava 66 na ambaye amewahi kuhudumu katika idara ya kilimo nchini kama afisa, anasema aliingilia kilimo cha hema baada ya kurambishwa sakafu na ufugaji wa kuku wa nyama kwa sababu ya kero ya chakula duni ambacho hakijaafikia madini yanayohitajika.
Ni hatua asiyojutia kamwe kwani ameingia kwenye daftari la wakulima wanaotatua uhaba wa nyanya Vihiga.
“Kiungo cha mapishi ambacho ni bei ghali eneo hili ni nyanya. Wakati zinakosekana kabisa, moja huuzwa hata zaidi ya Sh15 ilhali ni mashambani,” aelezea Bw Asava.
Kaunti ya Vihiga mashamba mengi yamesitiri kilimo cha mahindi, maharagwe, mtama na wimbi.
Pia, baadhi ya maeneo hukuzwa majanichai, matunda kama vile ndizi, mapapai, maembe na maparachichi pamoja na viazi vitamu na mihogo.
Kwa miaka mingi kaunti hiyo imekuwa ikitegemea nyanya kutoka Mlima Elgon, Uasin Gishu na eneo la Kati, jambo linalofanya zao hilo humo kuuzwa bei ghali.
Mwaka 2013 ndipo Bw Asava aliwekeza karibu Sh300,000 kwenye kivungulio chenye ukubwa wa mita 8 upana na mita15 urefu. Aidha, kimeundwa kiasi kwamba kina uwezo kusitiri minyanya 600.
Ndani, udongo umeinuliwa kuunda vipande sita, sawa na vitanda, kila kimoja kikiwa na mistari miwili inayopandwa mimea 60 katika kila mstari.
“Wateja wangu ambao wanajumuisha wa kijumla na rejareja, hujia mazao hapa shambani. Nyanya moja kubwa huwauzia Sh10, na zile ndogo huwafungia mbili au tatu Sh10,” afafanua.
Mkulima huyu anasema spinachi, kabichi na sucha humsaidia katika kuafikia kigezo cha mzunguko wa mimea (crop rotation).
Udongo wa Vihiga ni tifutifu nyekundu, na kulingana na Bw Asava kinachosababisha wakazi kutozalisha nyanya ni ukosefu wa maelezo au hamasisho. Wengi wameegemea dhana kuwa udongo na hali ya anga humo ni ya nafaka. “Maeneo yanayozalisha matunda, ni wazi kiungo kama nyanya kitafanya vizuri,” asema.
Katika suala hilohilo la ukosefu wa hamasa, afisa huyu wa kilimo wa zamani anasema wakulima wanaojaribu kukuza nyanya wamehangaishwa na ugonjwa aina ya Bacterial wilt, unaonyemelea minyanya na kuiacha ikikauka.
“Ugonjwa huu ni kero kwa mimea inayoorodheshwa katika familia moja na nyanya. Suluhu yake ni mkulima apande mbegu zinazoupiku, ambazo ni ghali,” aeleza.
Kulingana na Bw Benoit Montalegre, mtaalamu kutoka HM. Clause, kampuni inayozalisha mbegu za nyanya, mboga, matikitimaji na pilipili mboga, uhalisia wa mbegu ni suala analopaswa kutilia maanani mkulima.
Anasema sokoni kuna mbegu nyingi bandia na za hadhi ya chini zinazochangia mazao duni katika kilimo cha nyanya.
“Ufanisi katika ukuzaji wa nyanya unategemea uhalisia wa mbegu. Wakulima wanunue mbegu bora na zilizoidhinishwa na taasisi husika za kilimo nchini, la sivyo watakuwa wakishuhudia hasara,” anatahadharisha mtaalamu Montalegre.
Pembejeo
Kephis, ndiyo taasisi ya kiserikali inayojukumika kukagua ubora wa bidhaa za kilimo nchini.
Pembejeo zingine muhimu kutilia maaani ni mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, kwani soko lake pia limesheheni zile bandia.
Ili kukabili ugonjwa tata wa Bacterial wilt, baada ya mavuno katika kivungulio, mkulima anashauriwa kufunika udongo wote kwa karatasi nyeusi na asiruhusu mwanya wa hewa kuingia. Hilo linasaidia kuufurusha ikiwa ni pamoja na kuangamiza wadudu waliomo.
Bw Asava anasema kwamba tangu aanze kilimo cha hema hajawahi kupulizia mimea na mazao yake dawa dhidi ya wadudu.
Anafichua kuwa amegundua mmea aina ya ‘Mexican marigold’ ndio dawa murwa kufukuza wadudu.
“Huupanda kati ya minyanya na kadhaa kandokando mwa hema, sehemu ya ndani. Una harufu na sumu inayoangamiza wadudu,” akasema, akiongeza kwamba pia hung’oa kadhaa na kuwekelea kwenye minyanya.
Wadudu hatari kwa nyanya ni; nzi weupe, viwavi, vithiripi na Nematode.
Mmea huu wengi huuchukulia kama kwekwe, lakini mtaalamu huyu anasema ni mojawapo ya mbinu asilia kukabiliana na kero ya wadudu.
“Kilimohai kikitajwa, Mexican marigold inapaswa kujumuishwa ili kusaidia kukiafikia. Magonjwa sugu kama vile Saratani yanachangiwa na uzalishaji wa mazao kwa kutumia kemikali. Huhakikisha nyanya ninazozalisha ni salama,” afafanua mtafiti huyu.
Mkulima huyu pia hufuga kuku wa kienyeji na ng’ombe, ambao kinyesi chao hukitumia kama mbolea. Hutegemea maji ya mvua, ambapo huyaelekeza kwenye shimo na mengine kuyateka na kuyahifadhi kwa tanki.