AKILIMALI: Mradi unaosaidia shule kukimu mahitaji msingi
Na RICHARD MAOSI
TUNAKUMBANA na hema la kivungulio (greenhouse) tunapokaribishwa katika majengo ya shule ya wavulana ya Jomo Kenyatta inayopatikana katika eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru.
Shule ya Jomo Kenyatta inapatikana katika kipande cha ardhi cha ekari 54, ambapo usimamizi wa shule umeanzisha miradi mingi ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ng’ombe, samaki, ukuzaji wa mboga na utengenezaji wa lishe ya mifugo.
Ndani ya greenhouse tunakutana na Lilian Wangare, meneja wa kilimo na mwasisi wa mradi wa kukuza nyanya ndani ya kivungulio.
Anaambia Akilimali kuwa alianzisha mradi wenyewe mnamo 2015 akiwa na lengo la kupunguza gharama ya kununua nyanya kutoka kwenye soko la nje.
“Siku za hivi karibuni bei ya bidhaa imepanda sana, tukichukulia kwa mfano bei ya nyanya tulikuwa tukinunua kreti moja ya nyanya kwa Sh6,000 gharama ambayo hatuwezi kumudu tunapolisha zaidi ya wanafunzi 1600,” akasema.
Alieleza kuwa shule iliwekeza 500,000 katika miradi yote ya shule, ukuzaji wa nyanya ukiwa ni mojawapo ya miradi ambayo imestawi na kufanya vyema siku za hivi karibuni.
Lilian anasema mazao yakiwa ni mengi kupita kiasi huuza soko la nje, hususan wakati wa likizo wakati ambapo wanafunzi hawamo shuleni. Faida inayopatikana hutumika kuboresha mahitaji ya kimsingi ya shule kama vile kununua vyombo vya maabara, pamoja na kuboresha miundo msingi ya shule.
Shule ya Jomo Kenyatta hukuza aina ya nyanya zinayofahamika kama vile Anna F1, na kunyunyiziwa maji kupitia mtindo wa drip irrigation ambao ni bora kuliko aina nyingine ya kupokeza mimea maji na virutubishi muhimu.
Mtindo wa drip irrigation unapendwa miongoni mwa wakulima wengi kwa sababu kiwango kidogo tu cha maji ndicho kinachohitajika, ikizingatiwa kuwa kila mmea hupata maji ya kutosha.
“Kwa wiki moja tunaweza kuvuna zaidi ya kilo 150 za nyanya kiasi ambacho ni zaidi ya kile kinachohitajika kwa matumizi ya kila siku. Mazao yanayosalia huuzwa kwenye maduka ya kijumla mjini Nakuru,” akasema.
Mbali na kuwa mradi wa shule, nyanya zenyewe zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi wakati wa masomo ya kilimo ili kujiongezea ujuzi wa kilimo, kwa kufanyia uchunguzi.
Aidha wakati mwingine wanafunzi wamekuwa wakisaidia shule katika shughuli za kunyunyiza maji na kuvuna, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahami na ujuzi wa kutumikia kilimo wakiwa shuleni na hata likizoni.
Lilian anaamini kuwa mtu anaweza kujiajiri na kupata hela ndefu kutokana na ukuzaji wa nyanya, kwani ni mtaji kidogo tu unaohitajika katika hatua ya kwanza ya uzalishaji.
Lilian anasema nyanya zinapenda kukuzwa katika sehemu yenye kiwango kikubwa cha joto, ili kupunguza uwezekano wa mkurupuko wa maradhi yanayosababishwa na ukungu mwingi.
Ingawa tunda hili halipendi maeneo yenye mvua nyingi, maji ya kutosha ni jambo la kuzingatiwa. Aidha, joto la kadri husaidia kufanya matunda yaweze kuiva haraka na kupata rangi ya kijani kibichi iliyokolea.
Aliongezea kuwa nyanya hupenda udongo unaopitiza maji kwa urahisi na wenye rutuba ya kutosha, hivyo basi samadi inaweza kuongezewa ili kuinua kiwango cha rutuba.
Miche ya nyanya inaweza kukua kwa kuweka mbegu ndani ya kitalu, na huchukua baina ya siku 5-10 kabla ya kuanza kuchipuka.
Alisema kuwa kabla ya kusafirishwa shambani, miche huacha kumwagiliwa majii kwa siku mbili hivi ili ianze kuzoea hali ngumu katika mazingira mapya ya shambani.
Hatimaye ndani ya kitalu anasema nyanya hupandwa katika kina kirefu, ili iweze kutoa mizizi na kupata nafasi ya kunyonya maji ya kutosha iwezekanavyo.Vilevile nyanya hupata nafasi ya kutengeneza matunda ya hali ya juu.
“Katika majira ya jua kali mkulima anaweza kutandaza nyasi kwenye udongo, ili kupunguza kiwango cha unyevu kupotea kutoka kwenye mchanga,” akasema.
Licha ya kutumia mbolea za kawaida anawashauri wakulima kutumia mbolea kutoka viwandani ambazo huwekwa sentimita tano hivi kutoka kwenye shina la nyanya na huzunguka mmea mbolea kama vile CAN na NPK.
Mbolea inafaa kuwekwa mara mbili, kabla ya kukua na mara nyingine ni muda mchache tu baada ya kutoa maua. Hii husaidia kuifanya mimea ya nyanya kuendelea kutoa maua bila kuchoka.
Pia anasema kupunguza majani katika mmea wa nyanya ni jambo la kimsingi, kwa sababu husaidia kupunguza uwezekano wa mmea kusambaza maradhi kutoka kwenye tawi moja hadi katika tawi jingine.
Lilian aliongezea kuwa majani ya nyanya yanaweza kupunguzwa kwa njia ya mkono, ila mkulima asitumie kisu ama kifaa kingine chenye ncha kali kwani anaweza kupatia miche majeraha yanayoweza kusambaza maradhi kutoka kwa mche mmoja hadi mche mwingine.
Aidha anawashauri wakulima kujikita katika nyenzo za kukuza mimea pasipo kutumia kemikali ili kuzalisha mazao yenye afya tele kwa matumizi ya binadamu.
Lilian anaona kuwa utunzaji wa mimea unategemea utaratibu kwa kufuata kanuni za kitaaluma ili mkulima aweze kupunguza uwezekano wa kukadiria hasara kabla ya kufurahia mazao.