AKILIMALI: Vijana wabuni ajira kwa kusaga unga wa ndizi
Na PETER CHANGTOEK
CHINI ya umbali wa kilomita moja kutoka katika soko la Muthinga, katika wadi ya AguthiGaaki, kwenye uga wa chuo cha mafunzo anuwai cha Gathinga, mjini Nyeri, ndipo lilipo kundi la vijana lijulikanalo kama G-STAR.
Kundi hili lilituzwa kwa tuzo ya ‘mkulima bora’ katika maonyesho ya mwaka huu mjini Nyeri. Wanachama wa kundi hilo huzikagua, kupima uzani wa ndizi na kuzinunua kutoka kwa wakulima wanaoyawasilisha mazao hayo katika eneo hilo.
“Sisi huzinunua ndizi kutoka kwa wakulima kwa Sh12 kwa kilo moja, na kuzisaga kuwa unga,’’ adokeza Charles Wachira, 37, ambaye ni mwenyekiti wa kundi hilo, huku akitukaribisha kwa moyo mkunjufu.
Mnamo mwaka 2013, kundi hilo liligundua kuwa kulikuwako na uharibifu wa mazao ya ndizi baada ya kuvunwa katika eneo hilo, na wakaja na wazo la kuzuia kutokea kwa uharibifu huo. Hivyo basi, wakaamua kuboresha thamani ya ndizi kwa kuzikausha na kuzisaga kuwa unga, na hivyo kuzibuni nafasi za ajira.
Pindi tu ndizi zinaponunuliwa nao, husafishwa, na maganda huambuliwa na kukatwakatwa kuwa vipande vidogo na kusafishwa tena, kisha, ndizi hizo huwekwa kwenye kikausho cha sola. Kabla ndizi hizo hazijasagwa, kifaa fulani cha kupima hali ya unyevu hutumiwa kupima iwapo zimekauka ipasavyo.
Licha ya mafanikio ambayo kundi hilo limeyapata, hayakupatikana kwa urahisi.
Kundi lenyewe lilianzishwa na wanachama wanane tu, mnamo mwaka 2013, na mwaka mmoja baadaye, likaanza kuzitafuta hela za kuliwezesha kundi kuziendesha shughuli zake.
Mnamo mwaka 2015, lilipokea fulusi kutoka kwa mashirika matatu yasiyokuwa ya serikali. Lilipokea Sh50,000 kutoka kwa Uwezo Fund, Sh100,000 kutoka kwa Hazina ya vijana, Sh90,000 kutoka kwa shirika la USAID kupitia kwa mradi ujulikanao kama ‘Yes Youth Can Program’ na mnamo mwaka 2018, vilevile, likapokea Sh1.775 milioni kutoka kwa mradi wa Upper Tana.
Aidha, kundi hilo likapata mafunzo kutoka kwa asasi tofauti tofauti; mathalani Wambugu Farm, na chuo kikuu cha JKUAT kuhusiana na utengenezaji wa chakula.
Hata hivyo, changamoto kuu ikawa ni kutokuwa na shamba la kuendeshea shughuli zao, kwa sababu wanachama walipoomba fedha, mashirika yasingekubali kutoa fedha kwa mradi ambao ungeanzishwa katika shamba la mtu binafsi.
Jitihada za kulitafuta shamba zikaanza, na ikawachukua takribani miaka mitatu ili kulipata. Kwa wakati uo huo, wanachama sita wakaondoka kutoka kwenye kundi, na wawili tu ndio wakasalia. Jambo hilo likawashurutisha wawili hao kuwasajili wanachama wengine ili wapate ufadhili wa kifedha, la sivyo wangeambulia patupu.
Kundi hilo lilipewa kipande cha ardhi na serikali ya kaunti, katika chuo anuwai cha vijana cha Gathinga na shughuli za ujenzi wa kiwanda zikang’oa nanga.
Kwa sasa, kiwanda hicho kina vikausho vitatu vya sola, ambavyo hukausha kilo 400 kwa wiki moja.
Baada ya ndizi kusagwa, huchanganywa na unga wa mtama na mahindi kwa vipimo vya 1:1:2 (mtama, mahindi na ndizi mtwawalia). Unga uo huo uliochanganywa, hupakiwa na kuuzwa katika kaunti mbalimbali, kama vile; Nairobi, Nyeri na viunga vyake.
Kupunguza uharibifu
Agnes Muchiri, ambaye ni afisa aliyestaafu kutoka kwa Wizara ya Kilimo, katika kaunti ya Nyeri, anasema kuwa utengenezaji wa unga wa ndizi ni mojawapo ya mbinu za kupunguza uharibifu wa mazao baada ya kuvunwa shambani, huku virutubisho vilivyomo kwa ndizi mbichi vikisalia kwa unga huo.
“Unga huo una uwanga ambao husaidia utumbo kuwa na afya,’’ afichua mtaalamu huyo.
Ndizi zina manufaa mengi katika mwili wa binadamu. Zina madini aina ya ‘Potassium’, ambayo husaidia moyo kufanya kazi vyema, na pia husaidia mwili kutekeleza shughuli ya mmeng’enyo wa chakula (digestion) vizuri.
Pia, ndizi zina madini aina ya ‘Magnesium’, ambayo husaidia misuli na husaidia kuboresha usingizi kwa waja.
Isitoshe, zina madini ya zinki (Zinc), ambayo huimarisha kinga dhidi ya maradhi katika mwili wa mwanadamu.
Vilevile, ndizi huwa na madini aina ya fosforasi (Phosphorous), ambayo husaidia moyo kufanya kazi vyema mwilini.