ATHARI ZA PLASTIKI: Walaji samaki wa baharini wanajaza plastiki mwilini
Na LEONARD ONYANGO
UMEJITULIZA katika ufukwe wa bahari Hindi katika maeneo ya Mombasa, Kilifi au Lamu unakula samaki wa baharini huku ukiteremsha kwa mvinyo au maji ya chupa.
Bila shaka unaburudika, lakini wanasayansi wanaonya kwamba unajaza chembechembe za plastiki mwilini.
Baadhi ya samaki humeza mamilioni ya plastiki ambazo hutupwa baharini kila siku hivyo watu wanapowala, plastiki hizo huingia mwilini.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Victoria nchini Canada, sasa unasema kuwa walaji wa samaki wa baharini ndio wako katika hatari ya kumeza chembechembe nyingi zaidi za plastiki, ikilinganishwa na wenzao wanaokula samaki kutoka ziwani au mito.
Wanasayansi pia wanaonya kuwa wabugiaji wa mvinyo na maji ya chupa pia wanameza kiwango kikubwa cha chembechembe za plastiki mwilini.
Hata hivyo, wanasema kuwa bado madhara ya plastiki mwilini hayajulikani lakini wanaonya kuwa baadhi ya chembechembe ni ndogo kiasi kwamba huingia katika mishipa ya damu na kusababisha kinga za mwili kukosa nguvu.
Watafiti hao wakiongozwa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Victoria, Kieran Cox, walipima kinyesi cha watu kadhaa na kupata mamilioni ya chembechembe za plastiki.
Hata watu wasiobugia mvinyo, kunywa maji ya chupa au kula samaki wa baharini pia wanaingiza chembechembe za plastiki kupitia hewa.
“Tulibaini kuwa kupitia hewa mtu mzima hujaza chembechembe 50,000 za plastiki kwa mwaka huku watoto wakiwa na chembechembe 40,000 mwilini,” anasema Cox.
Vyakula vya kusagwa
Wanasayansi wanashuku kuwa vyakula vya kusagwa kama vile nyama, mboga na hata maziwa huenda pia vimesheheni chembechembe za plastiki.
“Katika utafiti wetu tulibaini kuwa maji ya chupa yana chembechembe za plastiki mara 22 ikilinganishwa na maji ya mfereji au kisimani. Mtu ambaye anakunywa maji ya chupa tu kila siku anaweza kumeza zaidi ya chembechembe 130,000 za plastiki kwa mwaka ikilinganishwa na 4,000 kwa mtu anayekunywa maji ya mfereji,” akasema.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa hivi punde inaonyesha kuwa zaidi ya watu 14,300 hufariki kila mwaka nchini Kenya kutokana na kupumua hewa chafu.
Kulingana na WHO, hewa chafu husababisha maradhi ya nimonia, kuhara kati ya magonjwa mengineyo. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto 600,000 walio chini ya umri wa miaka mitano hufariki kila mwaka kutokana na hewa chafu.
“Mazingira yaliyo na hewa chafu ni hatari sana kwa afya haswa miongoni mwa watoto wadogo. Huathiri kinga ya mwili hivyo kuwafanya kushambuliwa na magonjwa mengineyo,” ilisema ripoti hiyo.
Hata hivyo wataalamu wa matibabu bado hawajatambua athari za chembechembe za plastiki mwilini kupitia hewa.
Baadhi ya watafiti wanasema kuwa chembechembe za plastiki ambazo huingia mwilini kupitia hewa, hutolewa nje bila kudhuru mwili kupitia kukohoa au kupiga chafya.
“Kupiga marufuku vifaa vya plastiki vinavyotumiwa mara moja na kisha kutupwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira,” akasema Cox.
Umoja wa Mataifa (UN) unaonya kuwa plastiki zilizo na kemikali ya klorini huwa hata kwenye udongo na kwenye maji. Wanyama au binadamu wanapokunywa maji hayo, hudhurika.
Wataalamu pia wanasema plastiki zinapoyeyuka na kuwa chembe ndogondogo hutoa sumu ambayo huwa hatari kwa afya.
Kulingana na UN, plastiki hutoa kemikali zinazojulikana kama ‘phthalates’ na ‘Bisphenol A’ (maarufu BPA).
Kemikali hizo hudhuru homoni za miili ya wanyama na wadudu wengineo.
Kemikali hizo pia husababisha mwasho wa mwili na hata kudhuru mishipa ya damu ya ubongo na kitovu cha mtoto aliye tumboni.
Kenya ni miongoni mwa mataifa ulimwenguni ambayo yamepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.
Rais Uhuru Kenyatta majuzi alipiga marufuku matumizi ya vifaa vya plastiki vinavyotupwa baada ya kutumiwa mara moja kama vile vikombe, chupa za maji, vijiko na sahani karibu na mbuga za wanyamapori na fukwe za bahari. Ni marufuku ambayo huenda yakaanza kutekelezwa mwaka 2020.