• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Zuchu aomba radhi kwa onyesho ‘lisilofaa’

Zuchu aomba radhi kwa onyesho ‘lisilofaa’

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu alilazimika kuomba radhi baada ya mamlaka kusitisha shughuli zake zote za kisanii kwao visiwani Zanzibar kwa muda wa miezi sita kutokana na onyesho walilolitaja kuwa lisilofaa kimaadili.

Onyesho hilo lilifanyika Februari 24, 2024, katika kisiwa cha Kendwa,  Zanzibar.

Inadaiwa alitumia lugha isiyostahili na kwa wakati fulani alifanya ishara za kuashiria ngono.

Taasisi ya Sanaa ilisema maonyesho hayo yalikwenda kinyume na mila, desturi na utamaduni uliozoeleka hapo visiwani.

Mnamo Jumatano katika ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30, alisema Baraza la Sanaa nchini Tanzania (Basata) lilifanya kikao naye. Kikao hicho kikimpa mwelekeo kutokana na kazi yake ya sanaa.

Baadaye, mwanamuziki huyo aliomba msamaha kwa kosa lililotokea kutokana na uneguaji wake kwenye onyesho hilo.

Aliomba radhi kwa Watanzania huku akishukuru Basata kwa kuwa kielelezo chema kwa wasanii.

“Ninashukuru walezi wetu kwa kuniita na kufanya kikao nami na kunipa mwelekeo na mwongozo sahihi baada ya sanaa yangu kukiuka maadili yetu na utamaduni,” akasema Zuchu.

Kutokana na sitofahamu iliyotokea wakati wa onyesho hilo, mwanamuziki huyo alionekana kufahamu kosa ambalo alisema hakukusudia.

“Sintofahamu, iliyojitokeza kwenye shoo yangu ya pale Kendwa, niombe radhi kwa jamii… Lengo langu lilikuwa ni kuburudisha na sio kupotosha maana,” akaweka wazi.

Kulingana na lebo yake ya WCB Wasafi, Zuchu ni mwanamuziki wa kwanza wa kike kanda ya Afrika Mashariki kutazamwa kwenye mtandao wa YouTube kwa zaidi ya mara 500 milioni.

Zaidi na hayo, mwanamuziki huyo alipakia wimbo mwingine uliondamana na video iliyo na picha yake kwenye ukurasa wa Instagram, kuonyesha kuwa alijutia kitendo alichofanya.

  • Tags

You can share this post!

Ndovu Arsenal juu ya mti tena

KWPL: Bullets yanyoa Ulinzi bila maji, Kibera ikinyeshea...

T L