Akili MaliMakala

BSF ni siri kupunguza gharama ya ufugaji

Na RICHARD MAOSI March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA sababu ya gharama ya juu ya malisho wakulima wengi mijini na vijijini wamegeukia teknolojia ya kufuga wadudu aina ya Black Soldier Flies(BSF).

Wadudu ambao hutumika kama lishe kwa wanyama na binadamu. Protini inayotokana na wadudu hawa hutumika kama kiungo muhimu cha protini kwa ajili ya mifugo, nguruwe na kuku.

Kilimo cha BSF pia kina manufaa mengi katika utunzaji wa mazingira kwani husaidia kuchakata masalia ya lishe au mabaki ya wanyama.

Mildred Gachoka mkurugenzi wa Griincom Innovative Limited Nakuru, anasema si lazima mkulima awe na mtaji mkubwa ili kufanikisha shughuli yenyewe.

Kwa kutumia vyombo vyepesi kama vile beseni, mkulima anaweza kuunganisha zana hizi kwa ustadi mkubwa kutengeneza mazingira ya BSF kuzaana.

Mildred Day Gachoka, mkurugenzi wa Griincom Innovate Limited Nakuru akionyesha teknolojia ya kufuga wadudu Aina ya Black Soldier Flies (BSF). PICHA|RICHARD MAOSI

Katika hatua ya kwanza beseni hizi ambazo hutambuliwa kama eggies hupakwa rangi za kuvutia ili kuwavutia.

“Black Soldier Flies wanapenda kutua kwenye kifaa hiki cha eggies kinachtoa mazingira mazuri ya kuzaliana,” asema.

Anasema asilimia 50 ya wadudu hawa hutengeneza protini, 35 mafuta huku zaidi ya asilimia 10 inayosalia ikichukua virutubishi vinginevyo.

Wyclife Tanui mtaalam wa wadudu kutoka mjini Naivasha, anasema wafugaji wa kuku ndio wanalengwa zaidi kufaidika na teknolojia hii kwani wanaweza kutumia wadudu BSF kama malisho ya ziada.

Ni malisho ambayo yatawasaidia kuku kwa mfano kukua kwa haraka na kuyafikia mahitaji ya soko upesi.

“Ustawi wa teknolojia umekuja na faida nyingi kiasi kwamba siku hizi wakulima wadogo hawategemei lishe za kiasili tu kwa mifugo na kuku wao.”


Mildred Day Gachoka, mkurugenzi wa Griincom Innovate Limited Nakuru amekumbatia BSF kupunguza gharama ya ufugaji. PICHA|RICHARD MAOSI

Anawahimiza wakulima vijijini kukubali aina hii ya teknolojia kwa sababu itawasaidia kupunguza gharama ya kununua vyakula viwandani.

Kulingana na Tanui Serikali ya Kaunti na ile ya kitaifa zinafaa kushirikiana ili kuwafikia wakulima wadogo vijijini ambao hupata changamoto ya kufikiwa na lishe za kisasa.Anasema tayari kuna mafunzo ya Sayansi ambayo hutolewa na International Centre of Insect Physiology and Ecology (ICIPE) kwa lengo la kuwajuza wakulima namna ya kuandaa lishe zinazotokana na wadudu.

Pia, kuna hatua ya kukausha na hatimaye kuchakata BSFAnasema BSF ni wadudu ambao wanafaa kutunzwa katika sehemu inayokaa kama kizimba Isitoshe anasema kwa kutumia aina spesheli ya chombo ambacho huwa na kiwango sahihi cha nyuzi joto inaweza kumchukua mkulima baina ya siku 8-12 kwa wadudu wake kuwa tayari.

“Wakulima wengi katika kaunti za Kiambu, Nandi, Makueni na Machakos wanaendelea kufaidi kutokana na black soldier flies, yaani kilimo cha malisho ya bei nafuu,” asema.

Mbali na hayo wadudu wenyewe wanaweza kukaushwa , hatimaye wakatumika kutengeneza mafuta ya kupikia au unga.

Pia mtambo huu wa kufuga BSF unafaa kusafishwa kila wakati kuzuia maambukizi ya maradhi.

Anasema aina hii ya wadudu wanapokuwa wamefugwa kwa kutumia teknolojia sahihi, pia wanaweza kutumika kwa ajili ya kutengeneza mbolea asilia.

Vyumba vya kufuga BSF. PICHA|RICHARD MAOSI