MakalaSiasa

CECIL ODONGO: Raila na Ruto wasiamulie wananchi viongozi wao

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO ?

NAIBU Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga hawafai kutumia ushawishi wao wa kisiasa kuwaamulia raia viongozi ambao wanafaa wachaguliwe kwenye nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi wa 2022.?

Kuna mienendo inayoibuka ya viongozi hao wawili ambao wana ushawishi mkubwa nchini, kuwapendekezea raia viongozi hasa wale wanaofaa wapigiwe kura katika kiti cha ugavana.

Mnamo Alhamisi wiki iliyopita Dkt Ruto alimwidhinisha Waziri Msaidizi wa Leba Patrick Ole Ntutu kurithi kiti cha ugavana baada ya hatamu ya Samuel Ole Tunai kutamatika.

Naibu Rais alijigamba kuwa alitumia ushawishi wake serikalini kuhakikisha Bw Ntutu anapokezwa wadhifa anaoshikilia sasa baada ya kuanguka kura.

Kinachoshangaza ni kwamba Dkt Ruto hakuorodhesha miradi ya maendeleo ambayo Bw Ntutu aliwafanyia raia, alipokuwa Mbunge wa Narok Magharibi kabla ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana.

Kulingana na hotuba aliyotoa Dkt Ruto, huenda sababu yake kuu ya kumwidhinisha Dkt Ntutu ni kutokana na ukuruba ambao Waziri huyo msaidizi ameanza na mrengo wa Tangatanga baada kuonekana kukihama Chama cha Mashinani (CCM) ambacho alikitumia kupigania kiti hicho mnamo 2017.

Ni maendeleo gani makubwa ambayo Dkt Ntutu amewafanyia wakazi wa Narok kuliko wengine wanaomezea mate kiti hicho cha ugavana kama Katibu wa Wizara ya Ugatuzi Charles Sunkuli, mbunge wa Narok Kusini Korei ole Lemein, Seneta Ledama ole Kina na Mbunge Mwakilishi wa Kike Soipan Kudate.

Na je, iwapo hawa wote watataka kutumia chama cha Dkt Ruto kupambana na Bw Ntutu kwenye uteuzi je, watapata haki? Mnamo Agosti mwaka huu, Bw Odinga naye alimwidhinisha Gavana Profesa Anyang’ Nyong’o kutetea kiti chake kupitia ODM kwenye kura ya 2022.

Bw Odinga alisema kuwa Gavana huyo ametenda kazi ya kuridhisha tangu achaguliwe mnamo 2017 na anafaa muhula mwingine.

Ingawa kampuni mbalimbali za utafiti zimekuwa zikionyesha kuwa Profesa Nyong’o ni kati ya magavana wachapa kazi nchini, si haki kwa Bw Odinga ambaye ana historia ya kupigania demokrasia nchini kumpendelea gavana huyo.

Mtangulizi wa Profesa Nyong’o, Jack Ranguma na Seneta Fred Outa wanamezea mate kiti hicho na wana umaarufu mkubwa katika kaunti hiyo, huenda wakalazimika kuwania kiti hicho kama wawaniaji huru na kukipokonya ODM kiti hicho wakiungwa mkono na wapigakura wengi.

Hili suala la kuwaidhinisha viongozi ndilo limechangia kupungua kwa umaarufu wa ODM katika ngome zake huku wanaonyimwa tiketi wakiishia kushinda viti vyao kama wawaniaji huru.

Iwapo Bw Odinga na Dkt Ruto wameanza kuwaidhinisha viongozi sasa, basi kufikia 2022, watakuwa wametambua viongozi wandani wao kwenye ngazi zote za utawala katika maeneo yote nchini.

Hii itavuruga uhuru wa raia wa kujiamulia kutokana na ushawishi wao wa kisiasa.? Wakenya nao wanafaa wawe macho na kupiga msasa rekodi ya maendeleo ya viongozi wanaochaguliwa na iwapo hawatoshi mboga, basi wawatemwe debeni.

Kuna baadhi ya viongozi ambao waliingia madarakani kutokana na ushawishi wa kisiasa wa nyapara wa vyama vikuu lakini raia wengi wanajutia kuwapigia kura kutokana na uzembe na kutowawajibika kwao vyema.Kuwaidhinisha viongozi ni kama kurejesha Kenya kwenye enzi wa utawala wa chama kimoja.

Wakati huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Kanu Okiki Amayo ndio waliamua viongozi wa kuchaguliwa kwa kutumia mtindo wa kibaguzi wa mlolongo.

Bw Amayo na vibaraka wengine wa Kanu walihakikisha wanasiasa waaminifu kwa Rais Daniel Arap Moi ndiyo wanachaguliwa kupitia chama hicho.