Jamvi La SiasaMakala

Dalili hizi zinaonyesha demokrasia inabomoka Kenya

Na BENSON MATHEKA November 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UKURUBA wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, kutekwa kwa bunge na serikali na kutumia polisi kuzima wanaokosoa serikali ni dalili kwamba demokrasia nchini iko msalabani, wachanganuzi wa siasa wanasema.

Wanasema hatua hizi zote zimeua upinzani dhidi ya serikali kwa kuwa wabunge wanafuata maagizo kutoka kwa viongozi wa vyama vyao badala ya kuhoji iwapo wanachounga mkono kinaathiri haki za raia wa kawaida.

“Demokrasia ambayo nchi hii imekuwa ikifurahia iko hatarini. Haki za kikatiba na uhuru wa raia zimekandamizwa. Kukosoa serikali ni hatia inavyoonekana watu wakitekwa nyara kwa kujieleza. Hali ikiwa hivi, demokrasia hubaki katika maandishi pekee,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Katana.

Anasema matukio nchini katika miaka miwili iliyopita yanaonyesha ukiukaji mkubwa wa misingi ya demokrasia.

“Demokrasia tuliyozoea nchini tangu 1997 inabomolewa tena kwa kasi sana. Katika miaka miwili iliyopita, tumeshuhudia ukandamizaji mkubwa wa haki. Watu wanatekwa mchana na kuzuiliwa kwa zaidi ya siku 30 bila kufikishwa kortini.

“Wanateswa na vikosi visivyojulikana katika hatua ya kunyamazisha wanaokosoa serikali na haya yakitendeka, viongozi waliochaguliwa hawashinikizi haki za raia ziheshimiwe kwa sababu wamewekwa makwapani na wakuu wa serikali,” asema

Kulingana na Bw Katana, wanachozingatia wabunge ni maslahi yao ya kibinafsi na sio ya raia waliowachagua. Wanasahau kwamba hawatakuwa wabunge milele na baadhi ya mambo wanayopitisha huenda yakawaathiri wakiondoka katika nyadhifa zao kwa sasa.

Mchambuzi wa siasa Joseph Kisilu anasema ishara kuu kwamba demokrasia nchini iko hatarini ni miswada tata inayopendekeza  serikali au washirika  wa viongozi wakuu kama ule wa kuongeza muhula wa rais na viongozi waliochaguliwa na unaolenga kuamua Wakenya wanavyopaswa kuandamana.

Mswada wa kuongeza muhula wa viongozi waliochaguliwa umefadhiliwa na seneta wa Nandi na japo chama tawala na serikali imejitenga nao, wadadisi wa siasa wanasema ulinuiwa kupima hisia za raia.

Mswada uliofadhiliwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku, unalenga kuharamisha maandamano katika barabara kuu na maeneo mengine ya umma hatua ambayo Bw Kisilu anasema ni sawa na kuzima haki ya raia kukusanyika na kulalamika.

Viongozi wa kisiasa na wanaharakati wanaonya kwamba Mswada huo ni jaribio la kukandamiza haki ya kuandamana na kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali.

Seneta wa Kisii Richard Onyonka amekosoa Mswada huo, akisema kuwa unazima haki za Wakenya na kupatia serikali nguvu za kakamata wanaoikosoa.

“Mswada huu unataka kuharamisha maandamano, ambayo yanatambuliwa katika katiba,” alisema.

Kulingana na Bw Kisilu, mswada huo unakandamiza uhuru wa kujieleza ambao Wakenya wamehakikishwa katika katiba.

“Mswada huo sio wa kikatiba na serikali inalenga kuweka mipaka ya uhuru wa haki za raia. Ni kuua demokrasia ambayo raia wa nchi hii wamefurahia kwa miaka mingi,” akasema.

Anasema kuwa haya yote yanajiri kwa kuwa ukuruba wa Rais Ruto na Bw Odinga umewezesha serikali kuwa na idadi ya wabunge wa kuisaidia kupitisha miswada.

“Ukuruba wao uliomuondoa Rigathi Gachagua katika afisi ya naibu rais ni tishio kubwa la demokrasia katika nchi hii. Lililo wazi ni kuwa mradi tu viongozi wanatimiza maslahi yao ya muda mfupi hawajali mustakabali wa nchi na vizazi vijavyo,” asema Bw Kisilu.