• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
DAU LA MAISHA: Mafanikio ni bidii ya mtu, yake sasa inalipa

DAU LA MAISHA: Mafanikio ni bidii ya mtu, yake sasa inalipa

Na PAULINE ONGAJI

KWA wengi, ukaguzi wa hesabu ni mojawapo ya taaluma zinazohitaji utaalamu wa kipekee ambao kwa kawaida unatokana na mafunzo chuoni.

Lakini hayo ni masharti ambayo Nancy Mutuku ameweza kuyakiuka kwani kwa takriban mwaka mmoja sasa amekuwa akifanya kazi hii katika Easterbrook Company, Nairobi.

“Nilisomea maandalizi ya hafla (Events Organiser) kupitia mradi wa Kenya Youth Empowerment Opportunity Project (KYEOP). Kozi hii ilikuwa kuhusu jinsi mtu anaweza kupanga na kuandaa hafla ambapo madhumuni kuu yalikuwa kutuandaa kujitosa katika biashara,” asema Nancy.

Kwa kawaida kazi yake ya ukaguzi hesabu inahusisha kuhifadhi rekodi za kifedha na kuhakikisha kwamba ushuru unalipwa vilivyo na kwa wakati ufaao.

“Kazi yetu ni ya mikono kwani tunatumia vikokotoo vya kieletroniki (calculator). Ilinichukua muda kabla ya kuzoea vifaa hivi,” aeleza.

Ni kazi ambayo amejifunza kwa kuwatazama wenzake ambao walikuwa tayari kumrekebisha kila alipokosea. “Walinieleza mahali kila kitu kinapaswa kuwekwa ninapopewa mizania (spreadsheets) kufanya majaribio,” asema.

Aidha, kutokana na sababu kwamba hakuwa amesomea kazi hii chuoni, ilimbidi kusoma vitabu kibao ili kupata mwongozo.

“Pia, ili kujitambulisha vyema na kazi hii na kujua cha kufanya, ilinibidi kutafiti kazi zilizofanywa miaka ya awali katika shirika hili,” asema.

Japo bado hajapata fursa ya kushughulikia kampuni kubwa, ana fahari ya kutoa huduma zake kwa mashirika kadha, huku akitumai kwamba haitachukua muda kabla ya kuanza kukagua mahesabu katika taasisi za haiba ya juu.

Akizidi kusubiria wakati huo, pengine wengi watajiuliza ni vipi alipata ajira hii? “Niliipata baada ya rafiki yangu kunihimiza nitume ombi la kuomba kazi na bahati ikaniangukia,” aeleza.

Anasema kwamba japo ilikuwa bahati nzuri kwake, huenda mawazo yake chanya yalichangia.

“Mimi ni mtu mwenye mawazo chanya na niko tayari kuchukua fursa yoyote inayonijia. Ninapopewa fursa, mimi huhakikisha kwamba naitumia vyema,” aeleza.

Lakini haijakuwa rahisi kwa Bi Mutuku kwani amekumbana na changamoto sio haba. Anasema mwanzoni kazi zake zilikuwa na makosa mengi lakini amekuwa akiimarika taratibu. Aidha anasema wakati mwingine wateja huacha mapengo katika taarifa wanazowasilisha hivyo kutatiza ukaguzi wa hesabu.

Lakini hajaacha vizingiti hivyo kuzima azma yake ya kujiimarisha katika taaluma hii.

“Tangu nianze kufanya kazi sijawahi kusikia malalamishi kutoka kwa wateja. Kwa kawaida mtu hupewa miezi mitatu kufanya majaribio ambapo baada ya kukamilisha nilipewa fursa kushughulikia wateja,” aeleza.

Japo anajivunia kupenyeza na kuthibitisha uwepo wake katika taaluma hii, anasisitiza kwamba sharti arudi chuoni kuisomea zaidi kozi hii. “Aidha, ningependa kumiliki kampuni ya uhasibu na kutoa fursa kwa watu wengine kujifunza pia ili kuinua maisha yao,” asema.

You can share this post!

Waandamanaji wapinga mauaji ya raia nchini DRC

Yafichuka MCA mfu alilipwa marupurupu kwa...

adminleo