DHULUMA KWA WANAHABARI: Muthoki Mumo alivyoteswa na polisi wa Tanzania
Na PETER MBURU
IMEBAINIKA kuwa polisi wa Tanzania walimtesa aliyekuwa mwanahabari wa Nation Media Group (NMG), Muthoki Mumo, wakati alipozuiliwa pamoja na mtetezi wa haki za wanahabari mwenzake Bi Angela Quintal kutoka Afrika Kusini wiki moja iliyopita.
Kupitia makala aliyoandika Bi Quintal, Novemba 13, maafisa wa kitengo cha ujasusi katika taifa la Tanzania waliwazuilia kinyume na sheria walipokuwa wakifanya uchunguzi wao kuhusu visa vya vyombo vya habari kunyanyaswa na serikali.
Bi Quintal, ambaye ni mshirikishi wa programu ya Kamati ya Kulinda Wanahabari (CPJ) ya Marekani katika kanda ya Afrika, alifichua kuwa serikali ya John Pombe Magufuli imekuwa ikiendeleza unyanyasaji wa wanahabari katika taifa hilo, kiwango cha kuwanyima haki zao za kazi na kimsingi.
Wakati walipozuiliwa, Bi Quintal na Bi Mumo, ambaye alikuwa mwandishi wa gazeti la Business Daily walipokonywa vifaa vyao vya kazi kama simu na tarakilishi, huku Bi Mumo ambaye ni Mwafrika akiteswa kwa kuzabwa makofi na mmoja wa maafisa hao wa serikali.
“Tulianza ziara yetu ya siku 10 Tanzania mnamo Oktoba 31 kukutana na wanahabari, watetezi wa haki za binadamu na wanasiasa. Hii ilikuwa kwa ajili ya kuunda ripoti spesheli ambayo inafaa kuchapishwa 2019,” akaandika Bi Quintal.
Hata hivyo, licha ya kuwa wawili hao ambao wote wana asili katika taaluma ya uanahabari wamekiri kuwa walitimiza matakwa yote ya kuingia Tanzania, kutoa sababu za kwenda huko n ahata kupewa kibali na mamlaka inayosimamia mashirika ya habari nchini humo, haki zao zilikiukwa.
“Tulivamiwa katika vyumba vya hoteli tuliyokuwa nan a maajenti waliojidai kuwa maafisa wa uhamiaji. Pasipoti zetu na vifaa vya kielektroniki vilitwaliwa na tulinyimwa fursa ya kutafuta wakili ama maafisa wa ubalozi,” Bi Quintal akasema kwenye Makala hayo.
Aliendelea kueleza namna maafisa wa serikali walijaribu kuwanyamazisha, japo hali yao kuitisha usaidizi kutoka makao makuu ya CPJ, Marekani na kutumia mitandao ya kijamii kupiga kelele ikafanya dunia kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Wanaume hao walikuwa wakimlenga Muthoki kwa kuwa ni mwanamke mchanga na Mkenya. Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania umedorora miaka kadha iliyopita, kiwango cha serikali ya Kenya kulalamika.”
“Muthoki aliulizwa maswali kwa Kiswahili na kulaumiwa kuwa amewasaliti watu weusi na kuulizwa ikiwa kweli nilikuwa raia wa Afrika Kusini. Kuna mmoja haswa ambaye alikuwa akimtusi na kumtesa Muthoki. Hata alimzaba kofi na kumsukuma. Nilijaribu kuingilia lakini nikaambiwa nikae mbali,” akasema.
Alisema kuwa maafisa hao waliwapa uhuru tu takriban saa tisa alfajiri, baada ya mkubwa wao (ambaye alionekana kupokea amri kutoka juu) kuwaambia kuwa walikuwa huru kurejea katika vyumba vyao vya hoteli.
Hata hivyo, baadaye gazeti moja la Tanzania kwa jina Tanzanite liliripoti kuwa wawili hao hawakuwa wanahabari bali maafisa wa serikali ya nje, ripoti za kupotosha raia wa Tanzania ili kuficha ukweli wa mambo, wakati serikali ya nchi hiyo imelaumiwa kuwa inakiuka haki za wanahabari kupasha nchi ukweli way ale yanayoendelea.