Makala

DOMO KAYA: Ewe chipukizi kabla jina lako lijulikane, jipe miaka kama minane

February 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANAMIPASHO

MADAM Boss au ukipenda Akothee tumemzoea kwa posti za kuchamba hasa ukiwa wewe ni mkosoaji wake.

Lakini juzi kuna mawazo yake aliyoyamwaga pale Insta yakanigusa sana. Ishu aliyokuwa akizungumzia ilihusu gemu ya muziki hapa nchini.

Ni ishu ambayo binafsi nimepitia kama mwandishi. Katika posti hiyo, Akothee aliamua kutoa ushauri kwa wanamuziki chipukizi wenye pupa ya kutoka kimuziki. Bila ya kuwaficha, Madam Boss aliwachanua kwa ukweli mchungu. Sio rahisi. Tena sio rahisi katika nyakati hizi ambazo wasanii chipukizi wanaibuka kila kukicha.

Wasanii wengi chipukizi hujiamini sana, huamini uwezo wao unatosha kung’arisha nyota yao na siku moja.

Kwa miaka zaidi ya saba ambayo nimejishughulisha na uandishi wa burudani, mamia ya wasanii chipukizi wamewahi kunitafuta na kuniomba ‘sapoti’. Sapoti kwa maana ya mimi kuchapisha stori zao magazetini na mitandaoni. Wengi wao huamini kutokea magazetini kutatosha kuwafanya staa.

Na inapokosa kuwa hivyo, wengi hukata mawasiliano. Kuna wale nimeshawakatalia kitambo na kuwaambia bado wanahitaji muda.

Na ndicho alichoshauri Akothee. Kwa uketo aliwasihi wasanii chipukizi kujifunza kuwa na subra, wajipe muda. Muziki huwezi kutoka kwa siku moja. Kama tu walivyoimba Kleptomaniax, ‘Kabla jina yako ijulikane, jipe miaka kaa nane..”

Waulize wasanii kama Fena Gitu ambao walidumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka saba kabla ya kuja kutoka. Leo ni staa mkubwa. Khaligraph aliishi kwenye gemu kwa zaidi ya miaka saba kabla ya kuja kutoka na ndio sababu kila kukicha Omollo hataki kupumzika, anaachia madude kwa fujo.

Mwenyewe sasa hivi unaona alipo kutoka ubaunsa hadi staa. Wengi wa wasanii chipukizi wa sasa wanataka kuanza leo na wahiti kesho. Wanaishia kutumia fedha nyingi kurekodi video kali na audio wakiwa na matumaini makubwa kwamba mchakato huo utawageuza mastaa. Mwisho wa siku ndoto zao zinagonga mwamba wanaanza kunung’unika.

Akothee mwenyewe kawatolea mfano akikumbukia jinsi alivyotumia zaidi ya Sh4 milioni kurekodi video ya wimbo mmoja lakini kazi hiyo iliishia kupata views chini ya laki tatu kwenye Youtube.

Wasanii chipukizi sasa hivi wapo wengi, maprodusa nao wapo wengi na kwenye gemu hii, hamna tofauti na hekaya za Shamba la Wanyama. Unaliwa tu hamna wa kukuhurumia eti unaanza.

Maprodusa wenyewe siku hizi wapo wengi na kila mmoja ana njaa, kwa nini asimpotezee msanii chipukizi.

Kingine nilichogundua ni kuwa, wasanii wengi chipukizi hawajajifunza muziki biashara, wanaamini kuwa kama wakitoka na kuwa maarufu basi fedha zitaanza kuwaandama. Sio katika nyakati hii ambayo mastaa ni kibao.

Miaka ya nyuma wapo wasanii waliokula maisha kwa kijiko kutokana na kuwepo na ushindani mdogo. Sasa hivi kila mtu anaimba hadi bawabu wa kazini kwetu. Hamna cha raisi raisi kwenye gemu hii.

Wasanii chipukizi wajifunze kuwa na subra wanapoanza. Wasijikamue maziwa na damu kulazimisha kutoka hata ikiwa wanajiamini kivipi. Riziki ni mafungu saba kila mtu kaandikiwa yake na ndio sababu wanatakiwa kuwa na subra. Ikiwa Bandoocks walitoka mwaka jana na wewe chipukizi unaamini unapaswa kutoka kama wao, usilinganishe nyota yako, wajifunze kusubiri wakati wao utafika tu.