DOMO KAYA: Jameni tuacheni unafiki!
Na THOMAS MATIKO
MGALA muue na haki mpe. Kama kuna kipindi nilitarajia msanii Akothee angetrendi tena sana, basi ni wiki mbili zilizopita.
Mwafahamu kule Turkana na Baringo, Wakenya wamekumbwa na baa la njaa. Kuna ripoti kwamba watu 10 tayari wamefariki kutokana na makali ya njaa.
Naibu Rais William Ruto kakanusha kwamba hamna aliyefariki wakati uchunguzi wa vyombo vya habari umebaini kuwa ni kweli wapo watu waliotangulia mbele za haki kisa, njaa.
Yule chifu naye aliyeuza serikali kwa kutoboa ukweli huo kafutwa kazi kisa, eti ni mlevi.
Kenya yetu hii manzee, we acha tu. Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta iligundua Chifu ni mlevi baada yake kumwaga mtama?
Siku zingine hizo zote hakuwa mlevi? Nimewasikia baadhi ya watu mitandaoni wakidai kwamba kama basi Chifu huyo alifutwa kazi sababu ya ulevi, Rais naye anasubiri nini?
Nijuacho mimi ni hiki, kama akirudi Yesu Kristo leo na sharti la kwenda mbinguni iwe ni kusema ukweli, basi wapo watu wawili ambao watatua huko haraka. Mlevi na mtoto mdogo. Hawa kamwe hawawezi kudanganya.
Hivyo huyo Chifu mlevi wengi tumemwamini sana.
Hata nyie mnajua, ni wachache sana huamini kauli za Mheshimiwa Ruto.
Sitaki kwenda mbali, labda kwa kuwakumbusha tu.
Mnakumbuka akiwapa ahadi Harambee Stars kwamba angewapa Sh50 milioni wagawane endapo wangefuzu AFCON.
Na walipofuzu, ikawa taabu kutoa hela hizo? Ndiye yeye leo, katuambia hakuna aliyefariki njaa. Hehe! Acha nicheke kidogo.
Lakini kabla sijapoteza dira kwenye mada niliyoanza nayo, acha nirudi hapo hapo. Naulizaje jamani, hivi kwa nini Akothee hajatrendi? Nyie mabingwa wa kibodi, mnaopenda kuchamba mastaa hasa wanapoteleza, mlikuwa wapi kwa wiki mbili hizo zilizopita? Hivi hamkuona alichokifanya Akothee?
Mama huyo wa watoto watano aliguswa sana na janga hilo la njaa. Kuwaona wanawake wakiteseka na wanao kamwe hangevumilia.
Huyoo kwa haraka alianzisha harakati za kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwanunulia chakula na baada ya siku mbili tatu hivi alikuwa na Sh10 milioni kwenye akaunti.
Aliagiza chakula, kikapakiwa kwenye malori na kusafirishwa Turkana. Na kwa kuwa yeye ni madam boss, alipaa kwa ndege hadi Turkana akiwa na mafuta ya sun screen.
Si wajua tena kule jua ni kama vile limelipwa kuwaka tena likiwa limeteremka hadi levo ya paa la nyumba.
Na kwa alivyo mweusi kama wao tu Waturkana, aliogopa ngozi yake kukaangika kwa jua kali. Alijipaka mwili mzima, ungedhani Elianto vile, kisha akavalia mavazi yale ya Kiturkana ungedhania alikuwa kwenye harakati za kushuti upya ile filamu ya The Gods Must Be Crazy.
Wazi
Sehemu nyingi za mwili wake zilikuwa wazi, matiti yake kwa mfano yalionekana kuwa imara zaidi licha ya kunyonyesha watoto sita.
Hata ya baadhi ya slayqueens, kwa Akothee katu hayangefika bei.
Bado hawana watoto ila maziwa yao yamevutika kidogo nusra kufika kiunoni.
Sasa sijui itakuwaje watakapowapata watoto.
Kule Turkana, Akothee aligawa chakula kwa wahanga kwa siku kadhaa. Muda wote huu, wachambaji, nyie mabingwa wa kibodi ni kama vile hamkuwa na bundles kabisa. Au mwataka kusema hamkuziona picha hizo? Sikuona hata tusi.
Sasa nashindwa kuwaelewa, wakati akipanua miguu yake mkakesha kumdhihaki na kumchamba, bundles mlitoa wapi?
Au mlikuwa mumeokoa jahazi? Tuacheni unafiki. Kwa kizuri alichokifanya katu hamkuona kabisa. Naamini leo akirudia purukushani zake hizo mtamwamkia tena. Wanafiki wakubwa nyie, hata hamna aibu. Nkt!