Makala

Duale, Murkomen na Alice walivyoacha viti vya kisiasa kuteuliwa mawaziri

Na SAMMY WAWERU July 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TANGAZO la Rais William Ruto mnamo Alhamisi, Julai 11, 2024 kuvunja Baraza lake la Mawaziri lilitua kwa kishindo kwa taifa na ulimwengu.

Hata ingawa alisisitiza kuwa huduma za serikali zitaendelea kama kawaida, Rais Ruto kwenye hotuba yake alitangaza kutimua mawaziri wote.

“Chini ya mamlaka niliyopewa na Katiba (akinukuu vifungu), nimefuta kazi mawaziri wote,” akasema Dkt Ruto.

Mwanasheria Mkuu (AG) pia aliangukiwa na shoka la Rais, Mkuu wa Maziri, Bw Musalia Mudavadi (ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni) aliponea tundu la sindano.

Makatibu, hawakuathirika kutokana na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri wa serikali ya Kenya Kwanza ambalo limekuwa na idadi jumla ya mawaziri 24.

Liliundwa 2022, baada ya Dkt Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua kuchaguliwa kama Rais na Naibu Rais mtawalia.

Baadhi ya mawaziri waliotunukiwa ni wanasiasa, wakiwemo Waziri wa Ulinzi Aden Duale aliyehudumu kama mbunge wa Garissa Mjini, Bw Kipchumba Murkomen (Barabara) – Seneta wa Elgeyo Marakwet na Bi Alice Wahome (Ardhi), mbunge wa Kandara.

Mawaziri hao walilazimika kustaafu kutoka kwa nyadhifa hizo za kisiasa, ambazo walizihifadhi 2022.

Bw Duale, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, amekuwa kwenye ulingo wa kisiasa tangu 2007 ambapo alichaguliwa mara ya kwanza kuwakilisha eneobunge la Dujis (sasa Garissa Mjini).

Naye Bw Murkomen, alichaguliwa mara ya kwanza kama Seneta wa Elgeyo Marakwet 2013.

Sawa na Murkomen, Bi Alice Wahome aliingia bungeni kwa mara ya kwanza 2013.