Makala

Familia kuzika mifupa sita ya mzee aliyeuliwa na mwanawe katika mzozo wa mali

Na MWANGI NDIRANGU, BENSON MATHEKA September 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

USIKU wa Juni 25, 2024 ulikuwa wa kawaida kwa mzee Joseph Ndegwa maarufu kwa jina Ole Sota.

Baada ya kufurahia kinywaji alichopenda zaidi, alitoka kwenye baa aliyokuwa akitembelea mara kwa mara katika soko la Chuma na kupanda pikipiki kuelekea nyumbani kwake umbali wa mita 500 hivi.

Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho ya  Bw Ndegwa, 81, mjane aliyekuwa akiishi na mwanawe katika kijiji cha Njoguini kaunti ya Laikipia, kuonekana akiwa hai.

Hakujulikana alikokuwa hadi mifupa mitatu ilipogunduliwa kutoka boma lake na kufanyiwa vipimo vya DNA  na kuthibitisha  alikufa katika mazingira yasiyoeleweka.

Siku chache baada ya meneja huyo wa zamani wa kiwanda cha kahawa kutoweka, mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 56 alikamatwa kama mshukiwa mkuu na inasemekana aliungama kwa wapelelezi kuwa alimuua babake na kumzika kwenye kaburi la kina kifupi ndani ya boma hilo.

Kulingana na familia na wenyeji, baba na mwanawe waliokuwa wakiishi pamoja katika nyumba ya mbao yenye vyumba vitatu walikuwa wakigombana mara kwa mara kuhusu mali ya familia.

Katika ungamo lake, Bw Anthony Gitonga ambaye hajaoa, aliambia maafisa wa upelelezi kuwa babake alikuwa akipanga kuuza sehemu ya ardhi ya familia hiyo na tayari alikuwa ameuza ng’ombe wa familia hiyo kwa Sh41,000 kinyume na matakwa yake (mwanawe).

Ungamo hili lilisababisha idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na wapelelezi wa mauaji kuzuru boma hilo kufukua kaburi mnamo Julai 15, 2024 baada ya kupata agizo la mahakama.

Nyumba hiyo ambayo iko kwenye ardhi ya ekari nne imetangazwa kuwa eneo la uhalifu na ilikuwa chini ya uangalizi wa maafisa wa polisi wenye silaha kwa saa 24.

Hata hivyo, juhudi za kufukua mwili huo hazikufaulu kwani baada ya kuchimba futi mbili kwenye kaburi, hakuna kilichopatikana.

“Kulikuwa na maafisa wa serikali wapatao 100 wakiwemo maafisa wa afya ya umma na wapelelezi wa mauaji walioendesha zoezi la uchimbaji wa kaburi. Ni watu wa familia pekee waliokuwepo lakini ikabainika kuwa ndugu yangu alikuwa amewadanganya wapelelezi kuhusu kaburi lenye kina kifupi,” anakumbuka Bi Jeniffer Wanjiru Mungai, binti wa marehemu.

Kando ya kaburi hilo lililodaiwa kuwa na kina kifupi kulikuwa na vipande vya nguo na viatu vilivyoungua lakini hakukuwa na dalili za mwili wa binadamu.

“Kabla ya zoezi la ufukuaji, niliwahi kumtembelea kaka yangu katika Kituo cha Polisi cha Ngobit alikokuwa akizuiliwa na akanieleza siri kuwa alichoma mwili huo na kilichozikwa kwenye kaburi hilo lenye kina kifupi ni baadhi ya mifupa lakini polisi hawakupata chochote. Mifupa mitatu iligunduliwa ndani ya boma ikiwa imetafunwa na mbwa wa kuzurura,” aeleza Bi Mungai.

Wapelelezi na watu wa familia walipogonga mwamba kutafuta mwili wa mzee huyo waligeukia mifupa hiyo mitatu katika jitihada za kutegua hatma ya baba yao ingawa kwa mwonekano, ilionekana kuwa sehemu ya mifupa ya binadamu.

Wapelelezi walipeleka mifupa hiyo kwa Mwanakemia wa Serikali kwa uchunguzi wa DNA na mnamo Septemba 15, 2024, hofu ya familia ilithibitishwa; mifupa ilikuwa mabaki ya mzee huyo aliyepotea.

Familia ilipokuwa ikitafakari mipango ya mazishi, kazi ngumu iliyofuata ilikuwa kutafuta mabaki zaidi ya mwili ndani ya boma.

“Tulijadiliana na maafisa wa Serikali na majirani katika kutafuta mabaki mengine na baada ya kusaka mashamba sita ya jirani kwa muda wa saa tano, tulikusanya mifupa mitatu zaidi na kufanya idadi hiyo kufikia sita. Mifupa hiyo, yenye ukubwa wa chini ya futi mbili, ilikabidhiwa  polisi na kwa sasa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nanyuki,” asema Bi Eunice Muhindi, mjukuu wa Mzee Ndegwa.

Mifupa hiyo itawekwa kwenye jeneza na familia inasema itafanya mazishi, kwa kuwa vipimo vya DNA vilithibitisha kuwa alikuwa amefariki.

Itakuwa mwisho wa safari ya miezi mitatu ya kumtafuta mzee huyo ingawa kwa huzuni lakini bado ni afueni kwa familia.