FAUSTINE NGILA: Heko Twitter na Facebook kuzima tetesi za Trump
NA FAUSTINE NGILA
Katika uandishi wangu, nimekuwa nikiikemea mitandao ya kijamii kwa kuchangia pakubwa kwa kuenea kwa habari za kupotosha kutoka kwa watu maarufu na wenye ufuasi mkubwa.
Lakini raundi hii nataka kuipongeza mitandao hiyo, hususan Twitter na Facebook, kwa kujitokeza na kuwa ange kukabiliana na Rais wa Amerika anayeondoka Donald Trump ambaye amezoea kuchapisha cheche za maneno makali na jumbe za kupotosha zinazosomwa na mabilioni ya watumizi wa mitandao hiyo katika uchaguzi mkuu uliotamatika.
Bw Trump ana wafuasi wapatao milioni 88 kwenye mtandao wa Twitter na wengine milioni 32 katika ukurasa wake wa Facebook.
Pindi tu Amerika ilipoanza kuhesabu kura, Bw Trump alikuwa mwingi wa bidii kwenye mitandao hiyo akichapisha kila aina ya madai. Alisema kuna wizi wa kura, huku akijitangaza kama mshindi mtarajiwa katika kinyang’anyiro hicho cha urais.
Lakini baada ya kugundua njama zake, Twitter na Facebook hazikuchelewa. Zilimzima papo hapo kwa kueleza watumizi wa mitandao kuwa ‘habari hii haijathibitishwa na inapotosha.’
Hapo Jumanne bado Bw Trump alionyesha matumaini ya kutangazwa mshindi kwa kuchapisha kwenye akaunti zake za mitandao kuwa “tutashinda uchaguzi huu” na “kuna watu wanatumia vibaya fursa ya kuhesabu kura”, licha ya mpinzani wake Joe Biden kumiminiwa sifa na marais wengi dunia kwa kumbwaga.
Facebook iliwaeleza watumizi kuwa “Joe Biden ndiye Rais mtarajiwa baada ya uchaguzi kufanyika”, ujumbe ulioambatana na kila chapisho la Trump. Twitter nayo iliwashauri watumizi wake kuwa “madai haya ya wizi wa kura ni potovu”.
Kwa mara ya kwanza, nilifurahia hatua ya mitandao ya kijamii kuungana kupunguza kusambaa kwa habari feki, hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa taifa lenye uwezo mkubwa duniani, ambao ulifuatiliwa na kila nchi.
Hapo awali mitandao hii ambayo inategemewa sana duniani kwa habari za kuaminika imejipata pabaya kwa kusaidia kupotosha mamilioni ya watu. Facebook, kwa mfano, ilikuwa taabani hapo Julai baada ya kubainika kuwa ilishindwa kuzima habari feki kuhusu virusi vya corona, habari hizo zikifikia watu bilioni 3.8.
Lakini kilichofanya mitandao hii kuchukua uchaguzi huo kama jambo la kiusalama ni agizo kutoka kwa Bunge la Amerika, kuwa wiki mbili baada ya uchaguzi, kampuni hizo zitafika mbele yake kuelezea jinsi zililinda haki na demokrasia mitandaoni.
Ninaamini hatua hii italeta mwamko mpya katika uchaguzi wa taifa lolote lile, ikizingatiwa kuwa ni wakati wa kampeni na kupiga kura ambapo wanasiasa wana mazoea ya kutuma jumbe za kubadilisha maamuzi ya wapigakura.
Sasa ninasubiri kuona kampuni hizi mbili zikichukulia uchaguzi katika mataifa yanayoendelea kwa uzito zilizoonyesha, hasa hapa Kenya ambapo tayari kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 zimeanza.
Katika dunia ya sasa, demokrasia hufa katika giza la kidijitali, na ni wajibu wa wamiliki wa mitandao kulinda hali na ukweli, wapigakura wasije wakachagua viongozi wasiofaa.